Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka baadhi ya viongozi wa vijiji na kata wanaoshirikiana na wafugaji kuvunja sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kuwanyanyasa wakulima katika maeneo yao kuacha mara moja kufanya hivyo kwani viongozi hao wanakuwa wanashiriki katika migogoro kwa kuchonganisha wakulima na wafugaji.
Akizungumza jana (22.12.2020)
wilayani Liwale, kwenye kikao kilichoshirikisha wakulima na wafugaji wa Mkoa wa
Lindi kwa ajili ya kutatua kero zao, Waziri Ndaki amekemea urafiki wa baadhi ya
viongozi hao na wafugaji ambao umekuwa ukilenga kuwanyanyasa wakulima kutokana
na wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ya wakulima hao.
“Wakati mwingine mnawapa tabu
wakulima kwa sababu wafugaji wanashirikiana na hawa viongozi wetu wa ngazi za
chini kufanya mambo yasiyotakiwa sasa tuache, watendaji wa vijiji na kata
fuateni sheria, taratibu na kanuni mlizoelekezwa zinazopaswa kuwaelekeza katika
kutenda kazi zenu.” Amesema Mhe. Ndaki
Aidha, Waziri Ndaki
amefafanua kuwa siku zote wakulima na wafugaji zimekuwa ni jamii zinazoelewana
kwa sababu kila mmoja amekuwa akihitaji huduma kutoka kwa mwenzake, kwa maana
ya mazao ya kilimo na mifugo na kutaka uhusiano huo usiharibiwe na baadhi ya
viongozi wa ngazi za chini kuingia katikati yako kwa maslahi binafsi na kutaka
urafiki usio na tija kwa wakulima kati ya baadhi ya viongozi hao na wafugaji ufe
mara moja.
Pia, kuhusu sheria, taratibu
na kanuni za nchi waziri huyo amesema nchi haiwezi kuendeshwa kwa sababu jamii
moja ya watu wakali na wengine wapole bali lazima ifuate sheria, taratibu na
kanuni zilizopo kutokana na wakulima kulalamikia vitendo vya baadhi ya wafugaji
kuwa wakali wanapoingia katika maeneo yao na kulisha mifugo mazao ya wakulima.
“Tukifuata sheria itatusaidia
sana kuishi pamoja kama nchi wakulima na wafugaji fuateni sheria, taratibu na
kanuni zilizopo ili tuishi pamoja, na sheria zimewekwa na wawakilishi wenu
wabunge kwamba wananchi tukiwawekea utaratibu wa namna hii tunaweza kuishi kwa
amani na utaratibu.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki ameuarifu mkutano huo wa Mkoa wa Lindi kati ya wakulima na
wafugaji kuwa ni muhimu wafugaji kushirikiana na serikali katika kujenga
miundombinu ya ufugaji yakiwemo malambo ya kunyweshea mifugo yao maji kwenye maeneo
ambayo wamekabidhiwa na serikali kufuga mifugo kwa kuwa mahitaji ya wafugaji ni
mengi na hayawezi kukamilishwa na serikali pekee kwa mara moja.
“Mahitaji ya wafugaji ni
mengi wanahitaji malambo, malisho, majosho na minada haya yote kwa mara moja
inawezekana kabisa serikali isiweze kufanya kwa mara moja, ombi langu kwa
wafugaji ninaomba tushikiriane sisi wizara tunaweza kutengeneza michoro ya aina
ya malambo yanayotakiwa kuwepo ikiwemo gharama, lakini pia tunaweza kupata pesa
kiasi sasa naomba tushirikiane, wizara tukipata pesa kidogo tutawachangia nanyi
mtafute pesa kupitia umoja wenu ili tugharamie kwa pamoja hayo malambo kwa
kufanya hivyo itawezekana kabisa lakini mkubali nyinyi ni matajiri.” Amesema
Mhe. Ndaki
Ameongeza kuwa katika
kuhakikisha hilo linafanikiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaangalia kuanzia
bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya
kujengea malambo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuanzia na baadhi ya
vijiji kwa kushirikiana na halmashauri.
Akizungumza kwenye kikao
hicho kuhusu ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ngongo yaliyopo halmashauri ya
Manispaa ya Lindi, ambayo ameyatembelea siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi
Mkoani Lindi (21.12.2020) na kushuhudia kukamilika kwa ujenzi wa jengo la
machinjio hayo, ambapo inasubiri awamu ya pili ya ujenzi ya kuweka vifaa vya
kuchinjia na kuchakata nyama, Waziri Ndaki amesema ataongea na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani
Jafo, kuingiza bajeti ya awamu ya pili ya ujenzi huo kwa mwaka wa fedha
2021/2022 badala ya 2022/2023 ambapo ujenzi huo umewekwa sasa unaokadiriwa
kugharimu Shilingi Bilioni 2.5.
Waziri Ndaki amesema kwa kuwa
jengo la machinjio limekamilika ni vyema likamilike kwa kuwekewa vifaa mapema
ili machinjio hayo yaanze kufanya kazi na kuwanufaisha wafugaji kwa kuwa kwa
sasa mikoa ya Kusini ukiwemo Mkoa wa Lindi na Mtwara imeanza kupokea mifugo
mingi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, hivyo hitaji la mazao ya mifugo
litaongezeka na mkoa utaongeza mapato kupitia machinjio hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi amesema mkoa umeweka utaratibu wa kutenga maeneo
kwa ajili ya wafugaji ambao wamekuwa wakiingia katika mkoa huo, lakini
wanakabiliana na gharama kubwa katika upimaji wa maeneo hali iliyolazimu mkoa
kusitisha kupokea mifugo kwa sasa kwa kuwa maeneo yaliyotengwa ni machache.
“Tunaomba wizara ione namna
gani na TAMISEMI tunaweza kuja na mpango wa kuziwezesha halmashauri ili ziweze
kupima maeneo kwa kasi ambayo inaweza kusaidia kutosheleza mifugo kwa sasa hivi
niseme mheshimiwa waziri na ukweli kabisa tumesema tusipokee tena mifugo kwa
sababu hatuna pakuiweka, ardhi tunayo lakini hatuna sehemu tulizopima hivyo
mifugo ikija inakuwa vurugu na kukaribisha ugomvi kati ya wafugaji na
wakulima.” Amefafanua Mhe. Zambi
Mhe. Zambi pia amesema ni
muhimu kuangalia namna ya kudhibiti idadi ya mifugo kutokana na wafugaji kuwa
na mifugo mingi huku wakiendelea kuishi maisha duni na kutaka kuwepo na sheria
ya kudhibiti idadi ya mifugo.
Pia amekemea matumizi ya
silaha ya baadhi ya wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima
hali ambayo inatishia usalama wa wananchi wenzao na kuharibu mazao ya wakulima.
Nao baadhi ya wakulima na
wafugaji waliozungumza katika kikao hicho wamepongeza jitihada za Wizara ya
Mifugo na Uvuvi na Mkoa wa Lindi kwa kuwepo kwa mkutano huo kati ya wakulima na
wafugaji wenye lengo la kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuzitatua.
Wametaka wakulima na wafugaji
ambao watakiuka sheria, taratibu na kanuni zilizopo kwenye maeneo yao juu ya
maeneo ya wafugaji na wakulima wachukuliwe hatua za kisheria badala ya kuadhibu
kundi lote la jamii ya mtu mmoja aliyeshindwa kufuata sheria, taratibu na
kanuni.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Lindi ukiwa
ni mkoa wake wa kwanza nje ya Dodoma kufanya ziara mara baada ya kushika
wadhifa huo, akisaidiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza kwenye kikao kati ya wakulima na wafugaji Mkoa
wa Lindi kilichofanyika wilayani Liwale na kuwataka viongozi wa ngazi za chini
kutokuwa chanzo cha migogoro kati ya jamii hizo mbili. (22.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akipatiwa taarifa ya Mkoa wa Lindi na
mkuu wa mkoa huo Mhe. Godfrey Zambi wakati Waziri Ndaki alipofika katika Wilaya
ya Liwale kabla ya kuhudhuria mkutano kati ya wakulima na wafugaji ikiwa ni
siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi. (22.12.2020)
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi Bw. Rogers Shegoto akielezea umuhimu wa kuendeleza maeneo ya malisho kwa
kupanda malisho ya mifugo pamoja na kujenga miundombinu ya maji ili kudhibiti
migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, wakati wa
kikao cha wakulima na wafugaji Mkoa wa Lindi kilichofanyika wilayani Liwale.
(22.12.2020)
Muonekano wa wakulima na
wafugaji waliohudhuria kikao kilichofanyika wilayani Liwale Mkoani Lindi chenye
lengo la kutatua migogoro kati ya jamii hizo mbili, kikao hicho kimehudhuriwa
pia na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Lindi na viongozi wengine wa serikali ya mkoa
wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo Mhe. Godfrey Zambi ambapo mgeni rasmi alikuwa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki. (22.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni