Na Mbaraka Kambona, Manyara
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka wale wote wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa.
Gekul alitoa onyo hilo alipokuwa akiongea na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo Disemba 21, 2020.
Kwa mujibu wa Waziri Gekul katika operesheni ya kupambana na
uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema
halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali ili
kukomesha vitendo hivyo.
“Hatutavumilia jambo hili liendelee, Sisi kama Wizara tumesema
ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari
kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema
Gekul
Aliongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia
kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo
mengine.
“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili,
shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo nyavu haramu zikatupwe,
tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho ,” aliongeza Gekul
Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa kipaumbele cha serikali kwa
sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia Vizimba na Mabwawa jambo
ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza
umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu.
“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Halmashauri
waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa Vijana,
Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi
wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na
tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” alisisitiza Gekul
Katika hatua nyingine, Gekul aliwaagiza Wakurugenzi wa
Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia
leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la Serikali.
“Hili litekelezwe haraka, kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi
ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elekroniki kwa kufanya
hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” alifafanua
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange alisema kuwa
maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na watayafanyia kazi
kama ilivyoelekezwa ili sekta ya uvuvi mkoani humo iweze kupiga hatua
inayotarajiwa.
“Tutahakikisha wavuvi wote tunawafikia kwa lengo la kutatua kero
zinazowakabili lakini vile vile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni
ili serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,”
alisema Twange
Mwenyekiti wa Wavuvi, Halmashauri ya Babati, Iddi Hassani
alisema kuwa watafanyia kazi maelekezo na watahakikisha wanashirikiana na
serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi na wataendelea kupambana na
uvuvi haramu ili kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya uvuvi endelevu.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Pauline Gekul akisisitiza jambo kwa Muwakilishi wa Kampuni ya XIN SI
LU, Suvi Zeng (hayupo pichani) alipotembelea eneo la ufugaji wa Samaki kwa
kutumia Mabwawa la Kampuni hiyo lililopo Mkoani Manyara Disemba 21, 2020. Nyuma
yake ni Viongozi wa Serikali pamoja na Wananchi waliojitokeza kumpokea Naibu
Waziri huyo.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) akipokea samaki aina Sato kutoka kwa
Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi
alipotembelea eneo la Kampuni ya XIN SI LU kutoka China iliyowekeza
katika ufugaji wa Samaki kwenye Mabwawa Mkoani Manyara Disemba 21, 2020.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Msaidizi,
Ukuzaji Viumbe Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Imani Kapinga alipokuwa
akimpa maelekezo Mwakilishi wa Kampuni ya XIN SI LU, Suvi Zeng (katikati)
alipotembelea eneo la ufugaji wa Samaki katika Mabwawa la Kampuni hiyo Disemba
21, 2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni