WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina amezindua Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji
wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 na kutangaza kuzifumua na kuziibua tafiti
zote zilizofanywa na wasomi na
kutelekezwa kwenye makabati miaka ya nyuma na kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa
matumizi ili kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo.
Pia agenda hizo zitaleta
msisimko mpya wa kufanya utafiti nchini na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi
na maendeleo tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo tafiti nyingi
zilifanywa na kutelekezwa kwenye makabati na watafiti mbalimbali wakiwemo Wanafunzi
wa Shahada ya Uzamili (Masters Degree)
na Shahada ya Uzamivu (PHD) katika vyuo vikuu mbalimbali.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa agenda hizo kitaifa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),
Kampasi ya Mazimbu mjini Morogoro, Waziri Mpina aliziagiza Taasisi ya Utafiti
wa Mifugo(TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi(TAFIRI) kubadilika ili kufanya
tafiti kwa vigezo vilivyowekwa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta za
mifugo na uvuvi nchini.
Waziri Mpina alisema
chimbuko la kuandaliwa kwa ajenda hizo za utafiti ni baada ya kubaini kuwa ajenda
zilizokuwepo awali za Mifugo na Uvuvi zilishindwa kuibua na kuzitumia tafiti
zilizofanywa kuchochea mabadiliko kwenye sekta hiyo muhimu ya uzalishaji.
Pia ajenda za utafiti
zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuzitambua, kuziorodhesha
na kuzitumia tafiti zinazofanywa na Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili (Masters
Degree) na Uzamivu (PHD) lakini sasa ajenda za utafiti zilizozinduliwa zimeweka
utaratibu wa namna ya kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti za wasomi
hao.
“Haiwezekani tafiti za
wasomi wa kiwango cha juu kiasi hicho wanazozifanya wakati wa kukamilisha masomo
yao ziishie kupata alama za ufaulu na kutupwa kwenye makabati, Leo kila mhitimu
atalazimika kuandaa policy brief ambayo itawezesha watumiaji na Serikali
kurekebisha au kuandaa Sera na Sheria” alisema Waziri Mpina.
Aliongeza kuwa Ajenda za
Utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuweka Kanuni
ambazo zitahakikisha kuwa utekelezaji wa
ajenda za utafiti unafanyika, lakini ajenda za utafiti iliyotangazwa inaweka
Kanuni zitakazotoa mwongozo na usimamizi wa utekelezaji na wajibu wa kila mhusika.
Aidha Waziri Mpina
alibainisha kuwa ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu
wa kuwaunganisha Watafiti wa Mifugo na Uvuvi nchini, na hivyo kupelekea kila
mmoja kufanya utafiti kivyake hali iliyosababisha jambo moja kufanyiwa utafiti
na mtafiti zaidi ya mmoja na kukosa jukwaa la kuratibu na kuchambua tafiti
zinazofanywa nchini.
“Agenda ninayoizindua leo
inakwenda kujumuisha watafiti na wataalam mbalimbali waliobobea katika fani za
mifugo, uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ili kuyapitia matokeo ya utafiti,
teknolojia zilizoibuliwa
na utafiti na kuzisambaza
kwa watumiaji kwa manufaa ya Taifa” alisema Waziri Mpina
Pia Waziri Mpina
alibainisha mapungufu mengine yaliyomo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwepo za
Mifugo na Uvuvi ni pamoja na kutoweka msingi mzuri wa kusimamia Watafiti na
kufanya tafiti kulingana na mahitaji ya soko badala yake Taasisi za Utafiti na Watafiti kufanya tafiti
nyingi za nje na mambo muhimu ya wananchi yanayohitaji kufanyiwa utafiti
kutelekezwa.
“Leo hii agenda
ninazozizindua zimeweka utaratibu wa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, kupanua
mtandao wa utafiti na kufanya tafiti
zote kulingana na mahitaji ya wananchi.
Mfano katika maeneo ya nyama, maziwa, samaki, ngozi, chakula cha samaki
na mifugo, magonjwa, malisho na migogoro” alisema Mpina.
Aidha dosari nyingine
zilizokuwepo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi ni kutojumuisha
katika vipaumbele masuala mengi muhimu yenye changamoto nyingi ikiwemo Mitaala na hali ya ajira.
Mpina alisema mitaala
inapoanzishwa haifanyiwi utafiti wa mara kwa mara matokeo yake mafunzo yanayotolewa
sio yale yanayohitajika katika soko la ajira huku Wanafunzi wanaohitimu mafunzo
hawajulikani wanakwenda wapi baada ya kuhitimu na hakuna mfumo wowote wa
uratibu.
“Ukienda kwa wafugaji
wanaofuga na kuchunga sio hao waliosomea mifugo, ukienda kwa Wavuvi na Ukuzaji
viumbe maji wanaovua na kufuga si hao waliosomea taaluma hizo, ukienda
viwandani vilevile”alisema Mpina.
Pia Masoko na Biashara,
Uongezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi (Livestock and
Fisheries value chain value addition), agenda iliyopita ilizingatia uzalishaji
pekee bila kuangalia upande wa soko wakati vitu hivi vinakwenda kwa pamoja
kwani hakuna uzalishaji bila soko.
Waziri Mpina pia alisema
licha ya kushamiri kwa migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na
eneo hilo kugubikwa na changamoto nyingi
ikiwemo mifugo kutaifishwa,
kupigwa risasi, kufilisiwa, kuuwawa kwa watu na mifugo na kupigwa faini kubwa kiasi cha kutishia
uendelevu wa sekta lakini eneo hili halikujumuishwa katika Agenda ya utafiti
iliyopita.
Pia masuala mtambuka, afya
ya wanyama na magonjwa ya afya ya jamii (Zoonotic Diseases) ambapo hivi sasa
asilimia 60 ya magonjwa yasiyoambukiza yanatokana na mazao ya mifugo, malisho,
nyanda za malisho na vyakula vya mifugo na samaki, uvuvi endelevu katika maji
ya asili (Uvuvi Haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi) ambayo nayo hayakuzingatiwa katika agenda za
utafiti zilizopita .
Hivyo Waziri Mpina
aliwahakikishia watanzania kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wote
kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa zinawafikia walengwa kwa wakati
ili tafiti hizo ziongeze tija na kipato kwa watuamiaji na Taifa kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda alimhakikishia Waziri
Mpina kuwa kwa niaba ya watafiti wa Chuo kikuu hicho watatakwenda kuwa sehemu
ya utekelezaji wa agenda hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni