Serikali imewataka wafugaji
katika Wilaya za Chunya na Mbarali Mkoani Mbeya kufanya shughuli zao kwa
kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo ya kutoingiza mifugo katika maeneo
ya Hifadhi za Taifa ya Ruaha na Pori la Akiba la Ruangwa, hali ambayo imekuwa
ikisababisha migogoro kati ya wafugaji na askari wa Hifadhi za Taifa (TANAPA),
wanaolinda hifadhi hizo ambapo baadhi ya migogoro hiyo imesababisha vifo vya
wafugaji, askari na mifugo.
Akizungumza Jumanne hii
(19.11.2019) wakati wa kuhitimisha ziara ya siku mbili ya makatibu wakuu kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya
Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Sheria na Katiba, waliozuru baadhi ya
maeneo yenye migogoro katika wilaya hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza
mifugo katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya malisho kwa kuwa ni kinyume na
taratibu za nchi.
“Serikali inawataka
wafugaji wote kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na kutoingiza mifugo
katika maeneo ya hifadhi za taifa kwa kuwa ni kinyume cha sheria pia serikali itaendelea
kuhakikisha wafugaji wanafanya shughuli zao kwa amani bila kubughudhiwa ili
mradi wanafuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo ya kutoingiza mifugo katika
mashamba ya wakulima.” Amesema Prof. Gabriel
Akizungumza kwa niaba ya
makatibu wakuu wa wizara hizo, Prof. Gabriel amefafanua kuwa kutokana na Tangazo
la Serikali (GN) Na. 28 la Tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2008, ambalo liliongeza
eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutoka Kilometa za Mraba 5,878 hadi kufikia
Kilometa za Mraba 20,226 hali hiyo imesababisha eneo la malisho kupungua kutoka
hekta 259,000 za awali hadi 154,000 katika Wilaya za Chunya na Mbarali ambapo
amewataka wafugaji katika wilaya hizo kuheshimu tangazo hilo wakati serikali
ikifanyia kazi maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli ya kuainishwa kwa vijiji vilivyopo katika maeneo ya
hifadhi ili maboresho yaweze kufanyika kwa maslahi ya vijiji hivyo.
Katika ziara hiyo ya
makatibu wakuu kutoka wizara nne Mkoani Mbeya uongozi wa TANAPA umekubali kutengeneza
barabara za kuainisha mipaka ya maeneo ya hifadhi na vijiji mara baada ya
kuainishwa kwa mipaka mipya kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli la
kutambuliwa kwa maeneo ya vijiji na hifadhi za taifa ambalo tayari linafanyiwa
kazi.
Kufuatia matukio ya mauaji
ya askari mmoja wa TANAPA na askari mgambo mmoja mwaka 2018 waliouawa na
wafugaji wakati wakiswaga ng’ombe waliokamatwa katika Hifadhi ya Ruaha kuelekea
Kambi ya Nyota ya TANAPA iliyopo Wilaya ya Mbarali na tukio la hivi karibuni la
Tarehe 11 Mwezi Oktoba 2019 la kuvamiwa kwa kambi hiyo na baadhi ya wafugaji
wakiwa na silaha za jadi kwa nia ya kukomboa mifugo iliyokamatwa katika Hifadhi
ya Ruaha hali iliyosababisha kijana mmoja wa wafugaji (19) kupigwa risasi na
askari wa TANAPA na ng’ombe 14 kuuawa, Katibu Mkuu Prof. Gabriel amewataka wafugaji
kutumia njia zisizo halali kukomboa mifugo iliyokamatwa.
Akizungumza na baadhi ya
wafugaji katika Kijiji cha Igunda, Kata ya Igava Wilayani Mbarali, katibu mkuu huyo
amefafanua kwa wafugaji hao kuwa kutokana na sheria na haki za wanyama duniani
ni makosa kuua mnyama bila kuwa na sababu za msingi hali iliyosababisha serikali
kuchukua hatua kwa askari wa TANAPA waliohusika kupiga ng’ombe hao risasi na
hivyo kuwataka wafugaji hao kuwa watulivu kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa
na vyombo vya dola.
Aidha ameeleza kuwa kuwa
pindi mifugo inapokamatwa na askari wa TANAPA inapobainika kuingia kwenye
maeneo ya hifadhi, wamiliki wa mifugo hiyo wanapaswa kufuata taratibu za
kisheria za kulipa faini na kukabidhiwa mifugo yao na kusisitiza kuwa ni muhimu
kwa wafugaji kujiepusha kuingiza mifugo maeneo wasiyoruhusiwa yakiwemo ya
Hifadhi za Taifa.
“Sisi viongozi wa Wizara za
Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani ya Nchi na Sheria na Katiba
tunasikitishwa sana na matukio haya ya mauaji kijana mdogo amefariki dunia kwa
sababu ambazo zingeweza kuepukika kwa kutaka kumdhuru askari kwa kutumia silaha
za jadi akiwa na wenzake takriban 20 ili kukomboa ng’ombe waliokamatwa
hifadhini, tunawaomba mjiepushe na matukio ya namna hii fuateni sheria na
taratibu za nchi ili mfuge bila bughudha.” Amefafanua Prof. Gabriel
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwaongoza viongozi wenzake
katika ziara hiyo akiwemo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Bw. Ramadhan Kailima, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon
Mpanju na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha akimwakilisha
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda wamefika pia
katika Kijiji cha Lualaje Kata ya Lualaje Wilayani Chunya na kuzungumza na baadhi
ya wafugaji kufuatia matukio ya wafugaji hao kuingiza ng’ombe katika Hifadhi ya
Ruaha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima amewataka wafugaji hao kufuata
sheria na taratibu za nchi na kwamba jeshi la polisi litazidi kutoa ushirikiano
kwa wafugaji hao katika matukio mbalimbali yakiwemo ya kuwabaini baadhi ya wafugaji
ambao wamekuwa wakiingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja na kujihusisha
na uhalifu.
Naye Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Amon Mpanju amewataka wafugaji kuwa watulivu na
walitambue Tangazo la Serikali Na. 20 la Tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2008,
ambalo liliongeza eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kupunguza eneo la malisho
katika Wilaya za Chunya na Mbarali hali iliyosabisha baadhi ya maeneo
waliyokuwa wakiyamiliki kubadilishwa matumizi na kuwa ya hifadhi, ambapo suala
hilo tayari linafanyiwa kazi kwa maelekezo ya Rais Magufuli na kuwataka kutoingiza
mifugo yao katika eneo la hifadhi hadi serikali itakapotangaza maamuzi mengine.
Kuhusu kuainishwa kwa
mipaka kati ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na Pori la Akiba la Ruangwa,
akizungumza kwa niaba ya katibu mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi
wa Idara ya Wanyamapori kutoka katika wizara hiyo Dkt. Maurus Msuha amesema
serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha inatuma timu ya
wataamu katika maeneo hayo ili kuweka alama maeneo ambayo wananchi yanawatatiza
kufahamu mipaka ya vijiji na maeneo ya hifadhi ili kuondoa migogoro kati ya maeneo
ya wakulima na wafugaji na mipaka ya Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba la
Ruangwa.
Baadhi ya wananchi katika
Wilaya za Chunya na Mbarali waliopata fursa ya kuzungumza wakati wa ziara ya
makatibu wakuu kutoka Wizara za Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Mambo ya
Ndani ya Nchi na Sheria na Katiba wamesema wamefurahishwa na ziara hiyo na
kwamba watazingatia maelekezo waliyopatiwa ili kuhakikisha wanafuga kwa kufuata
sheria na kwamba watashirikiana na serikali ili kuwabaini baadhi ya wafugaji
wanaokiuka sheria na kuingiza mifugo katika maeneo ya Hifadhi ya Ruaha na Pori
la Akiba la Ruangwa.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wamefafanua kuwa wamefurahishwa kwa viongozi hao wa juu kutoka wizarani
kufika hadi katika maeneo yao na kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo
ya maji na malisho pamoja na kupata taarifa za matukio ambayo yamejitokeza
katika wilaya hizo kutoka mamlaka mbalimbali za serikali wakiwemo viongozi wa
serikali, wafugaji pamoja jeshi la polisi.
Awali kabla ya makatibu
wakuu hao kutembelea wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali, wamefika katika
Ofisi ya Mkuu wa Mbeya na kuwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Albert
Chalamila pamoja Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, ambapo Mhe.
Chalamila amewaambia serikali ya mkoa huo itaendelea kufanya kazi kwa kusimamia
sheria na kuwaasa viongozi wenzake wanapofika mkoani hapo kupata taarifa sahihi
ya mkoa kabla ya kufika katika maeneo mbalimbali kuzungumza na wananchi.
Aidha Mhe. Chalamila
amebainisha kuwa migogoro ya wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali ambao
wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi ya Ruaha na Pori la Akiba
la Ruangwa katika Mkoa wa Mbeya unatokana na wafugaji kuwa na mifugo mingi tofauti
na maeneo ya malisho, hali ambayo imekuwa ikiulazimu uongozi wa mkoa kutoa
elimu kwa wafugaji juu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa wafugaji kuwa na
ng’ombe wachache wanaoweza kuwapatia matokeo mazuri.
Ameongeza kuwa uongozi wa
Mkoa wa Mbeya utazidi kusimamia na kutoruhusu mifugo kuingizwa katika maeneo ya
hifadhi pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha
mkoa huo unakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Katika ziara hiyo ya
makatibu wakuu wanne Mkoani Mbeya, ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiambatana na Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhan Kailima, Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Sheria na Katiba Bw.
Amon Mpanju na Mkurugenzi
wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda, ilikuwa na lengo la kupata taarifa
sahihi ya hali ya wafugaji katika Wilaya za Chunya na Mbarali pamoja na kupata hadidu
za rejea ambazo wataalam watatumia katika kufanya mapitio na maboresho ya
Tangazo la Serikali (GN) Na. 28 la Mwaka 2008 ili iwe shirikishi na kupata
suluhu ya migogoro ya wakulima na wafugaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni