VIJANA 85 RUVUMA WAPATIWA MAFUNZO YA UWEKEZAJI NA UFUGAJI WA KISASA

 Vijana  kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya uwekezaji na ufugaji wa kisasa kupitia Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi, inayoratibiwa na Serikali kupitia  Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Agosti 3, 2026.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Afisa Uvuvi wa Mkoa, Bw. Basil Amuli, amewataka vijana kutumia kikamilifu mafunzo na mikopo watakayopata kwa kuanzisha na kuendesha miradi yenye tija itakayowawezesha kujiongezea kipato na kujiajiri.

"Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi, hivyo ni wajibu wa wanufaika kuhakikisha wanatumia fursa hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kupata matokeo chanya na kuwa mfano kwa vijana wengine." amesema Bw. Amuli

Aidha, amewahimiza washiriki kutekeleza kwa vitendo maarifa watakayoyapata wakati wa mafunzo hayo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya Wanufaika Kanda ya Kusini, Dkt. Justinian Lutatina, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia kwa ufanisi mikopo watakayopata kupitia Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi.

Vilevile ameeleza kuwa vijana hao wamepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa fedha na mapato, uanzishaji na uendeshaji wa miradi yenye tija pamoja na mbinu bora za ufugaji wa kisasa wa nguruwe, mbuzi na kuku ili kuwawezesha kuendesha miradi yenye tija na endelevu.

Dkt. Lutatina amebainisha kuwa wanufaika 85 kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma wanatarajiwa kunufaika na programu hiyo, huku kila mmoja akipatiwa maarifa yanayozingatia sekta ya mifugo aliyoichagua kuwekeza.

Pia amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mikopo yatasaidia kuongeza uzalishaji, kukuza ajira, kuinua kipato cha vijana na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo wamesema mafunzo  yamewapa maarifa mapya kuhusu ufugaji wa kisasa, usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya mikopo, huku wakieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.

Vijana hao pia wametoa wito kwa wenzao kujitokeza kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia mafunzo na mikopo ya uwezeshaji kiuchumi ili kujenga maisha bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD