TDB YAKARIBISHA VIONGOZI WA CHAMA CHA MIFUGO TANZANIA (TSAP), YAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA TASNIA YA MAZIWA

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imewakaribisha viongozi wa Chama cha Wataalam wa Mifugo Tanzania (TSAP) katika ofisi za Bodi, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchini.

Mkutano huo uliwakutanisha Viongozi hao chini ya  Mwenyekiti wa TSAP, Dkt. Zabron Nziku, pamoja na Msajili wa TDB, Prof. George Msalya, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Tasnia ya Maziwa na Sekta ya Mifugo kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano huo Septemba 24, 2026, Dkt. Zabron Nziku alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya TSAP na TDB, hususani katika maeneo ya kitaalam, utafiti, ubunifu na kubadilishana maarifa yatakayosaidia kuongeza tija na ushindani katika Tasnia ya Maziwa nchini.

Kwa upande wake, Prof. George Msalya alieleza kuwa TDB ipo tayari kuendelea kushirikiana na TSAP pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Mifugo katika kutafuta na kutekeleza mikakati itakayochochea ukuaji endelevu wa Tasnia ya Maziwa. 

Alibainisha kuwa ushirikiano wa kitaalam ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tasnia hiyo na kutumia fursa zilizopo kuongeza uzalishaji, ubora na upatikanaji wa maziwa nchini.

Aidha, mkutano huo umeweka msingi wa kuimarisha mahusiano kati ya taasisi hizo mbili kupitia utekelezaji wa shughuli za pamoja zikiwemo tafiti, uhamasishaji, mafunzo ya kitaalam, ubadilishanaji wa taarifa na uzoefu, pamoja na kushirikiana katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa maendeleo ya Tasnia ya Maziwa.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza nguvu katika juhudi za Serikali na wadau wa Sekta ya Mifugo katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa, kuongeza tija kwa wafugaji na wazalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kuongeza mchango wa Tasnia hiyo katika uchumi wa Taifa.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD