TAFIRI YASHIRIKI MAFUNZO YA PILI YA TEKNOLOJIA YA SATELAITI KATIKA SEKTA YA BAHARI NA UVUVI

Na Herry Kilele – TAFIRI, Dar es Salaam.

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imeshiriki  kufanya mafunzo ya Pili ya Matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti katika Sekta ya Bahari na Uvuvi yanayofanyika katika Hoteli ya Southern Sun, Dar es Salaam, kwa ushirikiano na Taasisi ya Korea ya Sayansi na Teknolojia ya Bahari (KIOST).

Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu katika matumizi ya teknolojia ya satelaiti kwa ajili ya utafiti, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na uvuvi.

Akizungumza Agosti 19, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uendelezaji Tafiti na Uratibu wa TAFIRI, Dkt. Mary Kishe, amesema rasilimali za bahari na uvuvi zina mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania, usalama wa chakula na lishe, ajira, maisha ya wananchi pamoja na maendeleo ya uchumi wa buluu.

Amesema rasilimali za bahari na uvuvi zinaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohusisha mabadiliko ya mazingira, tabianchi, mabadiliko ya hali ya bahari pamoja na shughuli za kibinadamu.

Dkt. Kishe, alibainisha changamoto hizo zinahitaji upatikanaji wa taarifa sahihi za kisayansi na matumizi ya teknolojia za kisasa ni suluhisho ili kuwezesha wataalamu kuelewa, kufuatilia na kusimamia kwa ufanisi rasilimali za bahari na uvuvi.

Amesema taarifa zinazopatikana kupitia teknolojia ya satelaiti zinaweza kusaidia kufuatilia hali ya bahari, kubaini maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa samaki, kufuatilia mazingira ya bahari na maeneo ya pwani, kutathmini mabadiliko ya hali ya bahari pamoja na kuboresha utafiti na usimamizi wa sekta ya uvuvi.

Dkt. Kishe aliwahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa ya mafunzo hayo ya siku tatu kwa kushiriki katika vipindi vya vitendo, kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na kushirikiana na wakufunzi pamoja na watafiti kutoka taasisi mbalimbali.

Aidha, amesisitiza umuhimu washiriki hao kuwa mabalozi  kwa kuhakikisha maarifa na ujuzi utakaopatikana katika mafunzo hayo unawafikia wataalamu wengine kupitia kushirikishana ujuzi watakaoupata huo katika programu za utafiti na shughuli za Taasisi zao.

Akihitimisha, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya TAFIRI, Dkt. Mary ameishukuru  KIOST kwa ushirikiano wake katika kuimarisha uwezo wa kisayansi na kitaalamu wa watafiti wa Tanzania kupitia ubadilishanaji wa utaalamu, teknolojia na maarifa ya vitendo katika matumizi ya teknolojia ya satelaiti kwenye utafiti wa bahari na uvuvi. KIOST, Kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.

Kwa upande wake, Bw. Keunyoung Kim, kutoka Taasisi ya Korea ya Sayansi na Teknolojia ya Bahari (KIOST), amesema ana furaha kukutana tena na wataalamu wa Tanzania wenginwao wakiwa ni wapya katika mafunzo hayo.

Akieleza lengo la mafunzo hayo si kutambulisha teknolojia ya satelaiti pekee, bali pia kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili waweze kutumia kikamilifu taarifa za satelaiti katika ufuatiliaji na utafiti wa bahari na uvuvi iki kuchangia uchumi nchini Tanzania.

“Lengo kuu la mafunzo haya si tu kutambulisha teknolojia ya satelaiti, bali pia kujenga wataalamu wa ndani ambao wanaweza kutumia kikamilifu taarifa za satelaiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa bahari na uvuvi nchini Tanzania,” amesema Kim.

Amesema katika kipindi cha siku tatu za mafunzo, wataalamu kutoka Korea watashirikiana na washiriki kutoka Tanzania kupitia mihadhara na mafunzo ya vitendo, yatakayowawezesha kupata uelewa mpana wa matumizi ya teknolojia hiyo.

Kim amewataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kushiriki katika mijadala, kuuliza maswali na kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka Korea.

Aidha, amesema anaamini maarifa yatakayopatikana katika mafunzo hayo yatakuwa na manufaa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya wataalamu hao, pamoja na kuchangia katika uendeshaji wa baadaye wa Kituo cha Matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti kitakachojengwa nchini Tanzania.

Taasisi zinazoshiriki Mafunzo hayo yanahusisha wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi (SOAF), Taasisi ya Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Taasisi ya Sayansi za Bahari (UDSM-IMS) Zanzibar pamoja na Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Mafunzo hayo yanaweka msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania na Korea katika maeneo ya sayansi za  bahari, teknolojia ya satelaiti, utafiti wa uvuvi na matumizi ya taarifa za kisayansi katika kufanya maamuzi.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD