SERIKALI YAWAHIMIZA WAWEKEZAJI KUTUMIA SAYANSI, TAFITI NA UBORA WA VIFARANGA KATIKA UFUGAJI SAMAKI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuwahamasisha wawekezaji katika sekta ya uvuvi kuzingatia matumizi sahihi ya Sayansi na Tafiti za uvuvi katika kusimamia ubora na uzalishaji wa vifaranga vya samaki ili kuwa na tija katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba..

Kauli ya Serikali imetolewa Agosti 10, 2026 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati wa ziara yake mkoani Mwanza kwenye Shamba la Ufugaji Samaki kwa Njia ya Vizimba  la Big Best Company Limited lililopo Ilemela mkoani humo.

Alieleza kuwa serikali kupitia wizara anayoisimamia inaendelea kuwahamasisha wawekezaji wakubwa katika sekta ya uvuvi kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika viwanda vya chakula cha samaki huku  na akasisitiza juu ya matumizi ya Sayansi, tafiti pamoja na vifaranga vyenye ubora katika ufugaji wa samaki.

"Wawekezaji wakubwa wa sekta ya uvuvi changamkieni fursa ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha vyakula vya samaki, sekta hii ya ukuzaji viumbe maji ndio inakuwa hapa nchini, ni lazima uzalishaji wenu uzingatie matumizi sahihi ya Sayansi na tafiti, sasa taasisi yetu ya utafiti TAFIRI ishirikiane na wawekezaji kufanya tafiti za ubora wa vifaranga vyetu nchini" amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Bashiru alieleza kuwa Serikali inakamilisha kanununi pamoja na sheria  ya kupiga marufuku kuvua, kuhifadhi, kusafirisha na kuuza samaki waliochini ya kiwango ambapo kwa sasa zoezi la utoaji wa elimu ya uvuvi endelevu kwa wavuvi linaendelea kabla ya kanuni na sheria hiyo kuanza kutumika.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya 'The Big Best Company Limited', Prof. Samwel Mchele Limbu amesema shamba hilo linauwezo wa kuzalisha vifaranga vya samaki milioni 8 na kwamba kampuni hiyo yenye thamani ya shilingi Bilioni 205 ina vizimba 250 vya kulelea samaki, vizimba 500 vya kuvunia samaki na tayari ipo kwenye mpango wa ujenzi wa Kiwanda  chenye uwezo wa kuzalisha tani 72,000 za chakula cha samaki kwa mwaka mkoani Mwanza.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. William Kafiti ameiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea na utambuzi na usimamizi mipaka ya maeneo ya uvuvi ili kuondoa migogoro baina ya watumiaji wa Ziwa Victoria, huku baadhi ya wananchi wamesema uwepo wa Shamba la ufugaji samaki kwa njia ya vizimba (TBB) sio tu umekuwa ukiwanufaisha kiuchumi bali pia  umekuwa ukiwasaidia kupatiwa huduma za kijamii.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Katikati)akitoa maelekezo baada ya kukagua uzalishaji wa Vifaranga vya Samaki katika shamba la Ufugaji Samaki kwa Njia ya Vizimba la The Big Best Company Limited wakati wa ziara yake mkoani Mwanza leo Agosti 10, 2026.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (watatu kulia) akigaua ghala la kuhifadhia chakula cha samaki katika shamba la Ufugaji Samaki kwa Njia ya Vizimba la The Big Best Company Limited wakati wa ziara yake mkoani Mwanza leo Agosti 10, 2026.

Baadhi ya Mabwawa  ya kufugia Samaki katika Shamba la Ufugaji wa Samaki kwa njia ya Vizimba la The Big Best Company Limited yanayotumika kwa uzalishaji wa samaki




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD