SERIKALI KUIMARISHA MIFUMO YA TAARIFA ZA MIKOPO KWA VIJANA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaimarisha mifumo ya taarifa na takwimu kuhusu mikopo na uwezeshaji wa vijana kiuchumi ili kuongeza usimamizi wa miradi hiyo na kuhakikisha inakuwa na tija iliyokusudiwa.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo leo, Agosti 17, 2026, mara baada ya kuwasili mkoani Kagera akitokea jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi na shughuli zinazotekelezwa na serikali, ikiwemo sekta ya mifugo na uvuvi. Akiwa Kagera, amekutana na Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, na kufanya naye mazungumzo yanayolenga kuendeleza sekta za uvuvi na mifugo.

Katika mazungumzo hayo, amesema mfumo mzuri wa taarifa na takwimu za utoaji wa mikopo kwa vijana utasaidia kuwa na usimamizi mzuri wa miradi ya uwezeshaji, lakini pia utaondoa upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu wenye nia ovu, hivyo akatoa rai kwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri na wizara kuwa na ushirikiano.

"Tunataka kuongeza usimamizi, hasa katika maandalizi ya taarifa na takwimu katika miradi ya uwezeshaji mikopo kwa vijana. Kwa hiyo, waheshimiwa wakuu wa mikoa, wilaya na wizara tushirikiane kutoa taarifa kwa vijana, kuwachambua sifa zao, kwa sababu kuna tatizo pia la udanganyifu," amesema Balozi Dkt. Bashiru.

Kuhusu wizi na utoroshaji wa mifugo, hasa maeneo ya mipakani ukiwemo Mkoa wa Kagera, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amehimiza viongozi wa maeneo husika, kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuhakikisha wanafanya kazi kama timu moja ili kubaini mianya inayosababisha utoroshaji wa mifugo ambao unaikosesha serikali mapato.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Erasto Sima, amesema mkoa huo unaendelea kushirikiana na wizara katika ufugaji wa samaki kwa kupandikiza kwenye maziwa kama vile Ziwa Ikimba, na mwamko wa vijana kuchangamkia fursa hiyo umeongezeka kutokana na matokeo ya moja kwa moja ya sekta hiyo.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Erasto Sima akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa walipokuwa kwenye mazungumzo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera leo Agosti 17, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa(Kulia) akizungumza na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia nia Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima kuhusu utekelezaji wa miradi ya serikali katika sekta za uvuvi na mifugo baada ya kuwasili mkoani humo leo Agosti 17, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akisaini Kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera baada ya kuwasili mkoani humo leo Agosti 17, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD