SERIKALI KUENDELEZA MPANGO WA KUTOKOMEZA MAGONJWA YA MIFUGO

Serikali imesema itaendelea kuratibu ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa miundombinu muhimu ya mifugo nchini, ikiwemo majosho katika Jimbo la Newala Mjini, ili kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe na mbung’o.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma leo Agosti 26, 2026 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani wakati akijibu swali la Mhe. Rashid Mohamed Mtima, Mbunge wa Newala Mjini, aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga josho la kuogeshea mifugo katika jimbo hilo.

Mhe. Kamani amesema Serikali inatambua umuhimu wa majosho katika kudhibiti magonjwa ya mifugo na kwamba imekuwa ikitekeleza mpango wa ujenzi wa majosho nchini tangu mwaka wa fedha 2021/2022.

"Serikali imeendelea kujenga na kukarabati miundombonu ya kuongeshea mifugo ambapo hadi sasa jumla ya majosho 754 yamejengwa nchini kote, kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 15.19." alisema Mhe. Kamani.

Amesema kwa sasa Serikali imejielekeza katika kutekeleza na kukamilisha miradi ya kimkakati, ikiwemo kuendelea na Mpango wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo nchi nzima, kwa lengo la kufikia azma ya kutokomeza magonjwa yenye athari kwa afya za wanyama na binadamu.

Aidha, ameitaka Halmashauri ya Newala Mjini kutumia sehemu ya mapato yake ya ndani kugharamia ujenzi na ukarabati wa majosho katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD