NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI AIPONGEZA FETA KWA KUSIMAMIA VIZURI MRADI WA BBT UVUVI
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Ng'wasi Kamani ameipongeza Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kwa kusimamia vizuri mradi wa BBT Uvuvi ambapo kwa hivi sasa vijana waliopatiwa mikopo isiyo na riba wanaendelea na ufugaji samaki kwenye vizimba katika Ziwa Victoria.
Mhe.Kamani ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la FETA kwenye maonesho ya nanenane kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma na kutaka kupatiwa maendeleo ya mradi wa vijana wa BBT Uvuvi.
Akitoa maelezo kwa Mhe. Kamani, Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani amesema hadi sasa FETA imeshapeleka vifaranga kwa asilimia 82 kwa vijana 168 wa Mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara, vijana wanaendelea vizuri na mradi ambapo wale waliopo Mwanza wanatarajia kuanza kuvuna samaki mwezi Oktoba mwaka huu.
"Hivi sasa samaki waliopo kwenye shamba la Nyegezi, Mwanza wamefikisha uzito wa wastani wa gramu 300 na wanatarajiwa kuanza kuvunwa mwezi Oktoba" alisema Dkt. Mzighani.
FETA ndio msimamizi mkuu wa mradi wa BBT Uvuvi, ambapo ina jukumu la kusambaza mbegu za samaki, chakula cha samaki, vifaa vya kufugia samaki pamoja na kutoa utaalamu wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.



Maoni
Chapisha Maoni