MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI BAHARINI KUTEKELEZWA NCHINI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinatarajia kutekeleza wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa uvuvi wa bahari utakaofanyika kwa mwaka mmoja na nusu hadi Januari 2028.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh mbali na kuahidi ushirikiano kwenye utekelezaji wa mradi huo amewataka wavuvi watakaoshiriki kwenye utekelezaji huo kuainisha yale wanayohitaji yaguswe na mradi huo.

“Kumekuwa na athari kubwa sana katika sekta ya Uvuvi kuanza kuharibika kwa matumbawe na hata joto la maji na ardhini limekuwa kubwa mpaka upatikanaji wa samaki umepungua hivyo tunaamini mradi huu utakuja kushughulikia na eneo muhimu sana kwa wavuvi” Amesema Prof. Sheikh.

Kwa upande wake mwakilishi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ambaye pia ni Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Bw. Salim Ahmed Hamza amesema kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa wavuvi waliopo visiwani Zanzibar ambapo pia utaunga mkono juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tulikuwa tunafanya mradi unaitwa “Inuka na uchumi wa buluu” kupitia fedha zilizokuwa chini ya mfuko wa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 na moja ya changamoto zilizoonekana wakati huo ni maeneo yaliyokuwa ya wakulima wa mwani na wavuvi waliokuwa wakivua karibu na pwani kuathiriwa na mabadiliko ya tabia hivyo Serikali ilitoa takribani boti 500 kwa lengo la kuwapeleka mbali zaidi ili waondokane na changamoto hiyo” Ameongeza Bw. Hamza.

Naye mwakilishi wa wavuvi hao Bw. Mohammed Kombo Hamad amesema kuwa uwepo wa mradi huo ni sehemu ya jitihada mbalimbali zinazoakisi dhamira ya Serikali kwa upande wao ambapo amekiri shughuli zao kuboreshwa zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Zanzibar zamani tulikuwa tunalalamika bei ya samaki ipo chini lakini leo kilo moja ya samaki kwa mvuvi anauza zaidi ya shilingi Elfu tisa hadi 10 na hiyo kwetu ni faida na fahari kubwa” Amesema Bw. Hamad.

Mradi huo unaotekelezwa kupitia shirika lisilo la Serikali la AGNES utafanyika kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itakuwa ni tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi, pili ni namna wavuvi wanavyokabiliana na athari hizo na awamu ya mwisho ni kujenga uwezo kuanzia ngazi ya watengenezaji wa sera hadi wasimamizi wa rasilimali za Uvuvi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh akizungumza na baadhi ya Wavuvi kutoka Tanzania bara na Visiwani Zanzibar, Watendaji wa Wizara za Mifugo na Uvuvi na ile ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kabla ya kuzindua mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa bahari Agosti 26,2026 jijini Dar-es-salaam.

Mtafiti wa Sera za sheria na bahari kutoka Shirika lisilo la Serikali la AGNES Bw. Fred Kung’u akieleza maeneo yatakayoguswa na  mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa bahari wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika Agosti 26,2026 jijini Dar-es-salaam.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD