MHE. MACHA AWATAKA VIJANA KUTUMIA MIKOPO KWA USAHIHI ILI KUJENGA UCHUMI IMARA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringa Macha, leo Agosti 5, 2026, amefungua mafunzo ya Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi na kuwataka vijana walionufaika na mikopo ya Serikali kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe chachu ya kujikwamua kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Macha amesema kuwa mafanikio ya vijana katika miradi ya mifugo na uvuvi yanategemea utayari wao wa kujifunza, kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia ushauri wa wataalamu. Amesema vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwa wataalamu wa mifugo pamoja na wafugaji wenye uzoefu wa ufugaji wa kisasa ili wapate maarifa na mbinu bora zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na kuendesha miradi yao kwa ufanisi.

"Ninawasihi mtumie mikopo hii kwa malengo yaliyokusudiwa na mjifunze kutoka kwa wataalamu wa mifugo pamoja na wafugaji wenye uzoefu ili muweze kuendesha miradi yenu kwa ufanisi. Msiwe na haraka ya kutafuta mafanikio, kwani yanahitaji uvumilivu, nidhamu na usimamizi mzuri. Pia, hakikisheni mnarejesha mikopo kwa wakati ili vijana wengine nao wanufaike na fursa hii iliyotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Mhe.  Macha.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, amewataka vijana kuhakikisha mikopo waliyopewa inatumika kikamilifu katika shughuli zilizokusudiwa, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa miradi ili kufikia malengo ya Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi.

Mafunzo hayo yanawawezesha wanufaika kupata ujuzi wa usimamizi wa miradi, matumizi sahihi ya mikopo pamoja na mbinu bora za uzalishaji katika sekta za mifugo na uvuvi. Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), yakilenga kuwawezesha vijana kujenga uchumi endelevu kupitia miradi yenye tija.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringa Macha, akizungumza na wanufaika wa Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi leo, Agosti 5, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Amewahimiza kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuendesha miradi yao kwa bidii ili kupata matokeo yenye tija.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, akizungumza na wanufaika wa Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi leo, Agosti 5, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Amewasisitiza kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kufanikisha utekelezaji wa miradi yao na kujiongezea kipato.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Bugomba akizungumza na wanufaika wa Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi leo, Agosti 5, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea vijana ujuzi wa usimamizi wa miradi, matumizi sahihi ya mikopo na mbinu bora za uzalishaji.

Afisa Miradi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Elias Gamba, akitoa mafunzo kwa wanufaika wa Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi leo, Agosti 5, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Mafunzo hayo yalijikita katika matumizi sahihi ya mikopo na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha uwekezaji wenye tija na endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringa Macha, ( katikati mstari wa mbele), akiwa katika picha ya pamoja na wanufaika wa Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi baada ya ufunguzi wa mafunzo yaliyofanyika leo, Agosti 5, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD