KAMATI YA BUNGE YAPOKEA TAARIFA ZA UTEKELEZAJI WA NARCO, TMB NA TDB
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Deodatus Mwanyika, leo Agosti 21, 2026 imepokea taarifa za utekelezaji wa majukumu kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika kikao kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Katika taarifa yake, Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imeeleza kuwa biashara ya nyama nje ya nchi imeendelea kuimarika, ambapo Tanzania imeingiza Dola za Marekani milioni 61.5 kutokana na mauzo ya nyama katika nchi 11.
Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 8.4, ikilinganishwa na mwaka uliotangulia huku, Nyama ya mbuzi imeongoza kwa kuchangia asilimia 67 ya jumla ya nyama yote iliyouzwa nje ya nchi.
Kwa mwaka 2025/2026, jumla ya tani 14,213.66 za nyama zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 61.5 ziliuzwa nje ya nchi, ikilinganishwa na tani 13,112.44 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 53.9 mwaka 2024/2025.
Kwa upande wa tasnia ya maziwa, taarifa imeeleza kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka lita bilioni 3.9 mwaka 2023/2024 hadi kufikia lita bilioni 4.2 mwaka 2025/2026, kiwango hicho ni sawa na asilimia 97 ya lengo la kuzalisha lita bilioni 4.3 za maziwa kwa mwaka.
Tasnia hiyo pia inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wananchi, ambapo inagusa takribani kaya milioni 4.6 na kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa zaidi ya Watanzania milioni 20.
Katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kampuni ya Ranchi za Taifa, (NARCO) imeeleza kuwa kampuni hiyo imendelea kununua ng'ombe na kuziboresha, uanzishaji wa ranchi ya Mwisa II pamoja na utekelezaji miradi inayolenga kuimarisha biashara ya mifugo lakini bado kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni, uvamizi wa maeneo ya ranchi.
Baada ya kupokea taarifaa hizo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika aliongoza waongoza wajumbe kujadili taarifa hizo ambapo pamoja na maoni na ushauri walioutoa kwa wizara na taasisi zake wajumbe pia walipongeza utekelezaji wa majukumu unaofanywa na taasisi hizo na kutoa maagio kuhusu namna bora ya kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.
Pia, Mhe. Mwanyika alisisitiza kuwa Wizara kwa kushirikiana na NARCO kutafuta njia madhubuti za uwekezaji katika ranchi za taifa, kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo inayokidhi mahitaji ya soko na uzalishaji, pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati na kuishukuru Kamati kwa maoni na ushauri iliyoutoa kwa Wizara pamoja na taasisi zake, huku akiahidi kufanyia kazi maoni na ushauri huo kwa lengo la kuendelea kuboresha utendaji na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo na uvuvi.






Maoni
Chapisha Maoni