FETA YAENDESHA MAFUNZO YA UTUNZAJI NA MATENGENEZO YA BOTI NA INJINI ZA UVUVI KATIKA MKOA WA TANGA

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) imeendesha mafunzo ya Utunzaji na Matengenezo ya Boti na Injini kwa Maafisa Uvuvi, Wahifadhi wa Maeneo Tengefu na wavuvi  wanufaika wa mkopo wenye masharti nafuu wa boti za kisasa za uvuvi zilizotolewa na Serikali.

Mafunzo hayo yamehusisha washiriki 22 ambao ni Maafisa Uvuvi wa Wilaya wanne (4) na wavuvi 15 kutoka Wilaya za Mkinga, Tanga Jiji, Pangani na Muheza, Afisa Uvuvi mmoja (1) kutoka Kituo cha FRP - Tanga na Wahifadhi wawili (2) wa Hifadhi ya Bahari - Tanga.

Mafunzo hayo ya siku 4 yalianza tarehe18 hadi 21 Agosti 2026 katika ukumbi wa Costal Zone mkoani Tanga.

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu FETA, Naibu Mkuu wa FETA Bi. Merisia Mparazo amewaasa wahitimu wa mafunzo kutumia ujuzi walioupata kuboresha shughuli zao za uvuvi na kusambaza elimu kwa wavuvi wengine ambao hawakubahatika kupata mafunzo haya.

Aidha amesema mafunzo haya yatapunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha usalama wa vyombo kwa kuondoa dosari za kiufundi zilizokuwa zikishugulikiwa bila kuzingatia kanuni za kitaalamu.

Kwa upande wake Afisa Tawala  Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Tanga Bw. George Mmbaga kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa amesema mafunzo haya yatawaongezea kipato wavuvi kwani kiasi cha pesa ambacho wangetumia kumpa fundi arekebishe injini kinaweza tumika kwenye mambo mengine.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Bahari Tanzania (TASFAM) - FETA Bw Arnold Mbunda amesema mafunzo haya yamewezeshwa na Mradi wa TASFAM unaotekelezwa katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi kwa  ufadhili na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Aidha, washiriki wa mafunzo wameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuiwezesha FETA kupitia mradi wa TASFAM kuwaletea mafunzo haya adhimu ambayo yamewapa uelewa wa namna ya kutunza na kutengeneza  boti na injini ambayo yanaenda kuwa chachu ya mafanikio kwenye utekelezaji wa majukumu yao kwa usalama na tija.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD