DKT. NCHIMBI AHIMIZA UBORA WA MIFUGO NA MASOKO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuwasisitiza wafugaji kuboresha Mifugo yao ili kupanua wigo wa soko la mazao ya Mifugo ndani na nje ya nchi.

Balozi Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Agosti 03,2026 wakati wa ziara yake kwenye mnada wa Mifugo uliopo kwenye viwanja vya maonesho ya kitaifa na kimataifa ya NaneNane vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma.

“Kwa mara ya kwanza nimejua kuwa na Mifugo nayo imefurahi hivyo nawashukuru kwa kazi kubwa mliyofanya na kwenye maeneo haya ya mifugo changamoto kubwa ni ubora wa Mifugo yenyewe na masoko kwa hiyo nadhani mnapojielekeza kwenye maeneo hayo mawili mnasaidia sana taifa letu”, Amesema Balozi Dkt. Nchimbi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amesema kuwa moja ya vitu ambavyo Wizara yake imejielekeza kwa sasa ni upatikanaji wa mbegu bora za Mifugo ambazo anaamini zitakuwa na tija kwa mfugaji ambapo zitawafanya kuwa na mifugo michache yenye uzalishaji mkubwa.

“Tunataka kupambana kuhakikisha kwamba tunawaweka wafugaji kwenye ramani ya uzalishaji wa kiuchumi na uchangiaji wa pato la Taifa ambapo tumeendelea kuongeza fedha kwenye kituo chetu cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) ili kupunguza gharama kubwa waliyokuwa wanaingia wafugaji ili kupata mbegu” Amesema Mhe. Kamani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwalisha samaki mara baada ya kufika kwenye mabwawa ya kufugia samaki yaliyopo kwenye eneo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Viwanja wa Maonesho ya kitaifa na kimataifa vya Dkt. John Samwel Malecelela jijini Dodoma Agosti 03,2026.





Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (Watatu kulia) akielezea mkakati wa serikali katika kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi alipotembelea vipando vya mifugo na uvuvi leo Agosti 03, 2026 katika Viwanja vya Dkt. John Malecela Jijini Dodoma.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD