DKT. MADELE: LISHE DUNI YA PROTINI NI CHANZO KIKUU CHA UDUMAVU

 Na. Stanley Brayton, WMUV

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, amesema ulaji mdogo wa vyakula vyenye protini ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia tatizo la udumavu, hususan kwa watoto, na kuwataka wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa zitokanazo na mifugo na uvuvi ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Dkt. Madele aliyasema hayo leo Agosti 7, 2026, katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi wakati wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika shughuli za kuhamasisha ulaji wa bidhaa za mifugo na uvuvi.

Alisema bidhaa zinazotokana na mifugo, samaki na viumbe wengine wa majini zina mchango mkubwa katika kuboresha lishe, ukuaji wa watoto, kuongeza ufanisi wa kazi na kujenga taifa lenye nguvu kazi yenye afya na tija.

"Taifa lenye wananchi wenye afya bora lina uwezo mkubwa wa kuzalisha, kubuni na kupunguza gharama za matibabu zinazotokana na magonjwa yanayozuilika kwa lishe bora," alisema Dkt. Madele.

Alisisitiza kuwa lishe bora ni nguzo muhimu katika kuboresha afya ya mama na mtoto, kupunguza vifo vya wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, pamoja na kupunguza tatizo la udumavu na ukuaji duni.

Akitoa takwimu za matumizi ya bidhaa za mifugo na uvuvi nchini, Dkt. Madele alisema kiwango cha ulaji bado hakijafikia viwango vinavyoshauriwa, na alieleza kuwa Mtanzania kwa wastani hula kilo 10.1 za samaki kwa mwaka badala ya kilo 20 zinazopendekezwa, kilo 18.4 za nyama badala ya kilo 50, mayai 132 badala ya 300, na lita 70.5 za maziwa badala ya lita 200 kwa mwaka.

Aidha, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi zinazowezesha maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi, zikiwemo bahari, maziwa, mito, mabwawa na nyanda za malisho, lakini fursa hizo bado hazijatumika kikamilifu kuongeza uzalishaji wa bidhaa za asili ya wanyama.

Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza wananchi kuwekeza katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mbuzi, ng'ombe wa maziwa, samaki, jongoo bahari, kilimo cha mwani na ukuzaji wa viumbe wengine wa majini ili kuongeza upatikanaji wa protini kwa gharama nafuu na kuboresha lishe ya familia.

Pia aliwataka wafugaji kushiriki kikamilifu katika kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo ili kulinda afya ya mifugo na kuhakikisha uzalishaji wa nyama salama na yenye ubora kwa walaji.

Vilevile, Dkt. Madele alisema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutekeleza programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kujiajiri kupitia sekta za mifugo na uvuvi kwa kuwapatia mafunzo, mitaji yenye masharti nafuu na usimamizi wa kitaalamu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, akihutubia na kuhamasisha wadau wa Sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, akitoa neno la utangulizi, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Picha ni wadau wa Sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (hayupo pichani), katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Afisa Uvuvi Mwandamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Fatuma Rajabu Juma (kushoto), akimuelezea Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (kulia), juu ya ubora wa bidhaa zitokanazo na mwani, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Picha ni wadau wa Sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo, wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kupata chakula kilichotokana na bidhaa za Mifugo na Uvuvi, baada ya kuhamasishwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (hayupo pichani) juu ya ulaji wa Vyakula vyenye protini, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, akilisha Samaki, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (wa tatu kushoto), akihamasisha uchanjaji wa Mifugo pamoja na utambuzi, katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Ngongo, wakati wa uhamasishaji wa ulaji wa bidhaa zitokanazo na Mifugo na Uvuvi, Agosti 7, 2026, Lindi.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD