DKT. KIMIREI AFUNGA MAFUNZO YA PILI YA TEKNOLOJIA YA SATELAITI KATIKA SEKTA YA BAHARI NA UVUVI
Na Herry Kilele – TAFIRI, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei, amefunga Mafunzo ya Pili ya Matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti katika Sekta ya Bahari na Uvuvi, yaliyolenga kuimarisha uwezo wa wataalamu katika matumizi ya teknolojia hiyo kwa ajili ya utafiti, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na uvuvi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika kuanzia Agosti 19 hadi 21, 2026, katika Hoteli ya Southern Sun, Dar es Salaam, kwa ushirikiano kati ya TAFIRI na Taasisi ya Korea ya Sayansi na Teknolojia ya Bahari (KIOST).
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Dkt. Kimirei amesema rasilimali za bahari na uvuvi zina mchango mkubwa katika uchumi, usalama wa chakula na lishe, ajira, maisha ya wananchi pamoja na maendeleo ya Uchumi wa Buluu nchini.
Amesema, Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira2050 ambayo inatambua utafiti na matumizi ya sayansi na teknolojia kama nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira2050. Amesema pia, kuwa anaamini maarifa na ujuzi walioupata washiriki kupitia mafunzo hayo utasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan katika utafiti, ufuatiliaji na usimamizi wa rasilimali za bahari na uvuvi, na hivyo kuchangia maendeleo ya sekta ya uvuvi na Uchumi wa Buluu nchini.
Dkt. Kimirei amesisitiza umuhimu wa washiriki kutumia maarifa waliyoyapata kwa vitendo katika Taasisi zao, pamoja na kuwashirikisha wataalamu wengine ili kuongeza wigo wa uelewa na matumizi ya teknolojia ya satelaiti katika Sekta ya Uvuvi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi (SOAF), Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Taasisi ya Sayansi za Bahari (UDSM-IMS) Zanzibar pamoja na Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
Mafunzo hayo yanaweka msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania na Korea katika maeneo ya sayansi za bahari, teknolojia ya satelaiti, utafiti wa uvuvi na matumizi ya taarifa za kisayansi katika kufanya maamuzi.
Aidha, mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani katika kutumia teknolojia za kisasa za satelaiti ili kupata taarifa muhimu kwa ajili ya utafiti, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na uvuvi nchini.



Maoni
Chapisha Maoni