DKT. BASHIRU: CHUO CHA KAOLE KITOVU CHA ELIMU YA KILIMO NA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amekitaja Chuo cha Kilimo na Mafunzo ya Mifugo Kaole kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani kuwa ni mfano wa mafanikio ya mageuzi kutoka kuwa eneo la harakati za ukombozi wa Afrika hadi kuwa kitovu cha kuzalisha wataalamu wa kilimo na mifugo wanaochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Akizungumza katika Mahafali ya Kumi ya Chuo hicho iliyofanyika leo Agosti 6, 2026, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru  alisema kabla ya kuwa taasisi ya elimu, eneo la Kaole lilitumika kama kambi ya mafunzo ya wapigania uhuru wa Msumbiji kupitia Chama cha FRELIMO  ambapo baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1975, eneo hilo lilikabidhiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye kusimamiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania kwa lengo la kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

"Kaole imebadilika kutoka kuwa kitovu cha mapambano ya ukombozi wa kisiasa na sasa ni kitovu cha mapambano ya maendeleo ya kiuchumi kupitia elimu inayolenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiri wengine" alisema Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika elimu ya ujuzi, sayansi na teknolojia ikiwa ni pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kwa kutambua kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea ubora wa rasilimali watu wake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndugu Ally Salum Hapi alisema chama hicho kitaendelea kukisimamia Chuo cha Kaole ili kuendelea kuzalisha wataalam wa sekta za kilimo na mifugo kwani sekta  hizo zinazowagusa wananchi wengi na zinaimarisha wa usalama wa chakula.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho Bw. Yeremiah Samson amesema tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2012, Chuo hicho kimekuwa kikizalisha wataalam  wenye weledi wa kuhudumu katika sekta  za uzalishaji wa Kilimo na Mifugo ambapo idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 33 wa mwanzo hadi zaidi ya 225 kwa sasa, huku risala ya wahitimu ikatoa mapendekezo ya kuboreshewa miundombinu ya kujifunzia kwa kuzingatia mageuzi ya teknolojia ili kuwa mafunzo yenye tija.

Aidha, Mahafali hayo yameenda sambamba na Uzinduzi wa Jengo la Kulala Wanafunzi waosoma chuoni hapo ambapo uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ambaye yeye binafsi aliahidi kutoa mifuko 200 ya Saruji na shilingi Milioni 2 na kisha kuendesha harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya kujifunza na kufundishia ili chuo hicho kiendelee kuzalisha wataalam wa kilimo na mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza wakati wa Mahali ya 10 ya Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani Agosti, 06, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa(watatu kutokea kulia) akiwa kwenye maandamano ya Mahafali ya 10 ya Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole Kilochopo Bagamoyo mkoani Pwani leo Agosti 06, 2026, kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa (Bara) Ndg. Ally Salum Hapi.

Wahitimu wa Stashahada ya Sayansi ya Mifugo kutoka Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole wakila kiapo cha kwenda kutumikia taaluma hiyo kwa wananchi Wakati wa mahafali ya 10 ya Chuo hicho kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani Agosti 6, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akikata utepe kuzindua Bweli la Wanafunzi Wavulana wakati wa Mahafali ya 10 ya Chuo hicho iliyofanyika leo Agosti 06, 2026 Bagamoyo Pwani.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa (Bara) Ndugu Ally Salum Hapi akizungumzia Jinsi Chama cha Mapinduzi kitakavyosimamia maendeleo ya Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole wakati wa Mahafali ya 10 ya chuo hicho iliyofanyika leo Agosti 6, 2026 Bagamoyo Pwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole cha Bagamoyo Mkoani Pwani wakati wa Mahafali ya 10 ya Chuo hicho leo Agosti 6, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD