CHUO CHA MAFUNZO YA MIFUGO KUJENGWA SAMUNGE NGORONGORO
Na. Stanley Brayton, WMUV
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) pamoja na kikundi rika cha jamii ya wafugaji wa kata ya Samunge (Erumasidai) wamekuja na Mkakati mpya wa kujenga Chuo cha Mafunzo ya Mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha elimu na huduma za kitaalam kwa wafugaji katika eneo hilo.
Chuo hicho kinatarajiwa kuwa kituo muhimu cha mafunzo kwa wafugaji, vijana na wadau wa sekta ya mifugo, kwa kuwapatia ujuzi wa kisasa kuhusu ufugaji bora, afya ya mifugo, lishe, uzalishaji pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji.
Akizungumza Agosti 24, 2026 Wilayani Ngorongoro jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kutembelea wafugaji wa eneo la Ngorongoro, Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt. Pius Lazaro Mwambene, amesema mpango huo unalenga kusogeza elimu ya mifugo karibu na wafugaji na kuhakikisha wanapata maarifa yatakayowawezesha kuongeza tija na kuboresha maisha yao.
Aidha, Dkt. Mwambene amesema Serikali imeridhia kikundi hicho kujenga Chuo kwani uwepo wa chuo hicho utasaidia kujenga kizazi cha wafugaji wenye uelewa mpana wa matumizi ya teknolojia na mbinu bora za ufugaji, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii katika hatua zote za utekelezaji wa mpango huo.
“Tunataka elimu ya mifugo iwafikie wafugaji moja kwa moja, kujenga chuo katika eneo hili kutatoa fursa kwa vijana na wafugaji kupata mafunzo bila kulazimika kwenda mbali kutafuta ujuzi, na lengo la Serikali ni kuona ufugaji unakuwa wa kisasa, wenye tija na unaozingatia mazingira,” amesema Dkt. Mwambene
Vilevile, Dkt. Mwambene amewapongeza wanakikundi hicho kwa kufikia uamuzi huo, na kuwataka wazingatie matakwa ya ujengaji wa Chuo hicho kwa kufuata taratibu zote za uanzishwaji Chuo, pamoja na uwepo wa uwepo wa madarasa, maabara ya Mifugo, kliniki ya Mifugo, Hosteli za wanafunzi, maeneo ya wanafunzi kujifunzia upandaji wa malisho, jengo la Utawala na sehemu ya kulia chakula na huduma ya kwanza.
Dkt. Mwambene amebainisha kuwa serikali itakuwa nao bega kwa pega katika kuhakikisha Chuo hicho kinakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi unaokidhi vigezo ili kuweza kutoa elimu Bora kwa Vijana na wafugaji.
Kwa upande wake, Kiongozi wa rika la jamii ya mfugaji wa Samunge (Erumasidai), Bw. Elisante Shoide, amesema wao kama wanakikundi wanahitaji uwepo wa Chuo hicho katika eneo hilo na wamejipanga vyema katika kujenga Chuo hicho ili kuacha alama na mazingira mazuri kwa wafugaji ili waweze kupata elimu ya kisasa ya ufugaji.
“Sisi wafugaji tunahitaji elimu na wataalam walio karibu nasi, na tukipata maarifa sahihi kuhusu afya ya mifugo, malisho na namna bora ya kufuga, tutakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yetu,” amesema Bw. Shoide
Bw. Shoide amesema uwepo wa chuo hicho utawapa vijana wa eneo la Ngorongoro fursa ya kupata ujuzi na ajira, huku ukisaidia kuongeza idadi ya wataalam wa mifugo wanaopatikana katika maeneo ya wafugaji.
Mpango huo unakuja wakati ambapo sekta ya mifugo nchini inaendelea kuhitaji wataalam na wafugaji wenye ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, magonjwa ya mifugo, changamoto za lishe pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Endapo mpango huo utatekelezwa, Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Ngorongoro kinaweza kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya kukuza ujuzi wa ufugaji na kuongeza tija kwa wafugaji katika eneo hilo na maeneo jirani.




Maoni
Chapisha Maoni