VIFARANGA VYA SAMAKI MILIONI 1.5 VYAPANDIKIZWA ZIWA RWAKAJUNJU - KARAGWE
◼️Bashungwa atoa pikipiki kwa Afisa Uvuvi wa Kata kuimarisha usimamizi.
Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuanza kunufaika na uchumi wa buluu kupitia zoezi la upandikizaji wa vifaranga milioni 1.5 vya samaki aina ya sato katika Ziwa Rwakajunju lililopo wilayani Karagwe.
Bashungwa ametoa shukrani hizo leo, tarehe 23 Julai 2026, katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandikizaji wa vifaranga vya samaki katika Ziwa Rwakajunju, iliyofanyika Kijiji cha Kafunjo, Kata ya Kamagambo, Wilaya ya Karagwe.
“Hili jambo halijawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru, Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake. Jambo hili linaenda kuleta mageuzi makubwa na kuongeza kipato cha wananchi wetu,” amesema Bashungwa
Bashungwa ameeleza kuwa zoezi la upandikizaji wa vifaranga linaenda kuleta mageuzi makubwa kwa wananchi na ameiomba Serikali kuongeza vifaranga vya samaki kufikia milioni 5 pamoja na kutoa boti ya kufanya doria katika ziwa hilo.
Bashungwa amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kufuata miongozo itakayotolewa ili kuwezesha vifaranga hivyo kukua na kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwanufaisha wananchi kupitia shughuli za uvuvi.
Aidha, ili kuendelea kusimamia kikamilifu rasilimali hiyo, Mbunge Bashungwa ameahidi kumpatia pikipiki Afisa Uvuvi wa Kata, ambayo itamwezesha kutekeleza majukumu yake ya usimamizi na ufuatiliaji.
Awali, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Nazael Madalla amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kukuza uchumi wa wananchi kupitia uchumi wa buluu, hususan uvuvi na ufugaji wa samaki.
Madalla ameeleza kuwa Serikali itaongeza vifaranga katika Ziwa Rwakajunju pamoja na kufanya upimaji wa ziwa hilo ili kubaini kama linafaa kwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Zaituni Msogfe ameishukuru Serikali kwa kuleta vifaranga milioni 1.5 vyenye thamani ya shilingi milioni 450.
Pia, Mhe. Zaituni amesema Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kuwezesha upimaji wa maeneo 12 ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba mkoani Kagera.





Maoni
Chapisha Maoni