NARCO YAZINDUA "BULLDOZER " KUIMARISHA SEKTA YA MIFUGO

 Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imezindua "bulldozer" lenye thamani ya Shilingi milioni 450 katika Ranchi ya NARCO Ruvu, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa Ranchi hiyo, na kuongeza upatikanaji wa malisho, maji pamoja na kukuza uzalishaji wa mifugo nchini.

Akizungumza Leo Julai 20, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NARCO, Balozi Dkt. Aziz Ponary Mlima, amesema ununuzi wa "bulldozer" hilo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya DIRA ya Taifa ya 2050, huku akibainisha kuwa litasaidia kukabiliana na changamoto za malisho na maji ambazo zinawakabili wafugaji nchini.

"Bulldozer hili litatumika kuchimba visima vya maji, kuondoa vichaka vinavyozuia ukuaji wa malisho na kutengeneza mipaka ya Ranchi ili kudhibiti uvamizi, na Ranchi hii ya NARCO Ruvu ndiyo ya kwanza kunufaika na matumizi ya mashine hii ambayo pia itasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji ndani ya ranchi za taifa." Amesema Dkt. Mlima

Balozi Dkt. Mlima ameongeza kuwa NARCO itaendelea kuwawezesha wawekezaji waliopo ndani ya Ranchi kwa kuwapatia huduma mbalimbali ikiwemo ukodishaji wa mitambo, hatua itakayoongeza tija ya uzalishaji na kuchangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali. 

Pia, Dkt. Mlima amewahimiza wafugaji kuwekeza katika mbegu bora za mifugo, madume bora, teknolojia ya uhimilishaji na matumizi ya viini tete ili kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mohamedi Zuberi Mbwana, amesema malengo makuu ya ununuzi wa "bulldozer" hilo ni kuongeza na kuboresha nyanda za malisho, kukuza uzalishaji wa nyama kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kusaidia wafugaji kukabiliana na changamoto za malisho wakati wa kiangazi.

Aidha Mkurugenzi Mbwana, ametoa Rai Kwa wafugaji na wawekezaji kutumia "Bulldozer" hilo la NARCO ili waweze kubadili mfumo wao wa ufugaji Kwa kupanda malisho na kuondoa  vichaka. Vilevile Serikali imeazimia kuongeza tani za uuzaji wa nyama nje ya nchi kutoka tani 14000 Kwa sasa mpaka tani 50000 ifikapo mwaka 2030, NARCO inajukumu la kuongeza uuzaji huo wa nyama nje ya nchi.

Naye, mmoja wa wawekezaji katika Ranchi ya NARCO Ruvu, Bw. Mbambile Kisanjo, ameipongeza Serikali kwa kuleta "bulldozer" hilo akisema litasaidia kuboresha upatikanaji wa malisho, kutatua changamoto za mipaka, kuondoa vichaka na kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, mambo ambayo yataongeza tija kwa wawekezaji na wafugaji wanaotumia ranchi hiyo.

Uzinduzi wa "bulldozer" hilo unaonyesha dhamira ya Serikali kupitia NARCO katika kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya ufugaji ili kuongeza tija, uzalishaji na mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa taifa, sambamba na kufanikisha malengo ya DIRA ya Taifa ya 2050.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Balozi Dkt. Aziz Ponary Milima (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa "bulldozer" lenye thamani ya Shilingi milioni 450 katika Ranchi ya NARCO Ruvu. Uzinduzi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa malisho na maji, kuboresha miundombinu ya ranchi pamoja na kuongeza uzalishaji wa mifugo nchini. Hafla hiyo ilifanyika Julai 20, 2026 katika Ranchi ya NARCO Ruvu, mkoani Pwani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Balozi Dkt. Aziz Ponary Mlima, akizungumza na wawekezaji waliopo katika Ranchi ya NARCO Ruvu wakati wa hafla ya uzinduzi wa "bulldozer" lenye thamani ya Shilingi milioni 450, lililonunuliwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa malisho na maji, kuimarisha miundombinu ya ranchi na kuongeza uzalishaji wa mifugo nchini. Hafla hiyo ilifanyika Julai 20, 2026 katika Ranchi ya NARCO Ruvu, mkoani Pwani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mohamedi Zuberi Mbwana, akizungumza na wawekezaji wakati wa hafla ya uzinduzi wa "bulldozer" lenye thamani ya Shilingi milioni 450 katika Ranchi ya NARCO Ruvu. Amesema ununuzi wa bulldozer hilo unalenga kuongeza na kuboresha nyanda za malisho, kukuza uzalishaji wa nyama kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kusaidia wafugaji kukabiliana na changamoto za ukame na kiangazi. Hafla hiyo ilifanyika Julai 20, 2026 katika Ranchi ya NARCO Ruvu, mkoani Pwani.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD