NAIBU KATIBU MKUU WA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI AIPONGEZA TALIRI KWA UTOAJI ELIMU YA UFUGAJI SABASABA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa namna ilivyojipanga kutoa elimu ya ufugaji na kuonesha teknolojia mbalimbali za kisasa katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Prof. Sheikh ametoa pongezi hizo leo, Julai 4, 2026, alipotembelea banda la TALIRI na kujionea shughuli mbalimbali za uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya mifugo. Amesema jitihada zinazofanywa na Taasisi hiyo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwafikishia wafugaji teknolojia na maarifa yatakayosaidia kuongeza tija, uzalishaji na maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.
Akizungumza katika banda la TALIRI, Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia, Bw. Gilbert Msuta, amesema Taasisi imejipanga kuhakikisha wananchi na wadau wanaotembelea banda hilo wanapata elimu kuhusu teknolojia mbalimbali zilizobuniwa kupitia tafiti za TALIRI.
Bw. Msuta amesema kuwa teknolojia hizo zinahusisha malisho na mbegu bora za malisho, mbari bora za mifugo, vyakula vya ziada vya mifugo, pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa kupima ubora wa maziwa na mabaki ya dawa kwenye maziwa ili kuhakikisha usalama wa chakula na afya ya walaji.
Aidha, Bw. Msuta ametoa wito kwa wananchi na wadau wa sekta ya mifugo kutembelea banda la TALIRI ili kujifunza teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo na kuchangia maendeleo ya uchumi wa wafugaji na taifa kwa ujumla.

Maoni
Chapisha Maoni