IDARA YA UVUVI YAKUSANYA SHILINGI BILIONI 39.6 ZA MADUHULI KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026

Idara ya Uvuvi iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekusanya Shilingi bilioni 39.6 za maduhuli katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni ongezeko kutoka Shilingi bilioni 32 zilizokusanywa katika mwaka uliopita, na mafanikio hayo yametokana na zoezi maalum la ufuatiliaji wa ukusanyaji wa maduhuli lililolenga kuimarisha ulipaji wa tozo stahiki, kuzuia utoroshaji wa mazao ya uvuvi na kuhakikisha utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za uvuvi nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kikao kazi cha utoaji wa taarifa ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa maduhuli kilichofanyika Julai 4, 2026, jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu wa Wizara hiyo (Uvuvi), Prof. Mohamed Sheikh, alisema kiasi kilichokusanywa kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 ni Shilingi bilioni 39.6, ambapo mwaka jana kiasi kilichokusanywa kilikuwa bilioni 32 tu.

Alisema zoezi hilo lilitekelezwa katika kanda mbalimbali za uvuvi nchini, zikiwemo Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Pwani, Kanda ya Ziwa Victoria pamoja na maeneo ya mipakani ya mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.

Prof. Sheikh alisema ongezeko hilo linaonyesha kuwa hatua zilizochukuliwa na Wizara katika kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli zimeanza kuzaa matunda, huku zikiendelea kuongeza mapato ya Serikali.

"Kwa kipindi cha Machi hadi Juni 2026 pekee tumekusanya Shilingi bilioni 16.1 kutokana na tozo za mazao ya uvuvi, usafirishaji wa mazao hayo pamoja na faini mbalimbali. Kwa mwaka wa fedha 2026/2027 tunalenga kukusanya Shilingi bilioni 71.5 za maduhuli," alisema Prof. Sheikh.

Aliongeza kuwa mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa (GDP) umeongezeka kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 2.2, huku ukuaji wa sekta hiyo ukiongezeka kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia 6.3 kutokana na kuimarishwa kwa usimamizi na utekelezaji wa sheria na kanuni za uvuvi.

Kwa mujibu wa Prof. Sheikh, tathmini ya Wizara imebaini kuwa ufuatiliaji wa karibu wa ukusanyaji wa maduhuli umeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa, na alisema wastani wa makusanyo ya kila mwezi umeongezeka kutoka Shilingi bilioni 2.9 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026 na kufikia Shilingi bilioni 4.02 kwa mwezi kati ya Machi na Juni 2026.

Aidha, alisema Wizara imeweka mikakati mipya ya kuhakikisha malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yanafikiwa katika mwaka mpya wa fedha, huku akielezea kuwa tathmini hiyo itaendelea kufanyika katika sekta ya uvuvi na baadaye kupanuliwa katika sekta ya mifugo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Prof. Sheikh alifafanua kuwa shughuli za ukusanyaji wa maduhuli zinahusisha ukaguzi wa mazao ya uvuvi yanayosafirishwa, ufuatiliaji wa usafirishaji katika maeneo ya mipakani, usimamizi wa utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi pamoja na utoaji wa elimu kwa wadau.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohamed Sheikh, akizungumza na Wataalam wa Wizara hiyo, katika Kikao kazi cha Utoaji Taarifa za Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya Idara ya Uvuvi kutoka Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Julai 4, 2026 Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohamed Sheikh (kushoto), akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa Kanuni na Sheria katika Ukusanyaji wa Maduhuli kwa Wataalam wa Wizara hiyo, katika Kikao kazi cha Utoaji Taarifa za Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya Idara ya Uvuvi kutoka Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Julai 4, 2026 Dar es Salaam, kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Nchini, Dkt. Baraka Sekadende.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Nchini, Dkt. Nazael Madalla, akitoa mapendekezo, katika Kikao kazi cha Utoaji Taarifa za Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya Idara ya Uvuvi kutoka Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Julai 4, 2026 Dar es Salaam.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Christian Nzowa, akitoa  mapendekezo, katika Kikao kazi cha Utoaji Taarifa za Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya Idara ya Uvuvi kutoka Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Julai 4, 2026 Dar es Salaam.

Picha ni Wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakijadili na kutoa mapendekezo juu ya Ukusanyaji wa Maduhuli, katika Kikao kazi cha Utoaji Taarifa za Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya Idara ya Uvuvi kutoka Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Julai 4, 2026 Dar es Salaam.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI