DKT. MADELE AVUTIWA NA JUHUDI ZA SEKTA BINAFSI UTEKELEZAJI DIRA 2025-2050
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Fabian Madele amevutiwa na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na sekta binafsi kwenye kutafsiri kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050.
Hayo yamejiri wakati wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda cha kusindika maziwa cha Kilimanjaro na Shamba la Mwekezaji binafsi la kuzalisha malisho na maziwa la NURU mkoani Arusha Julai 18,2026 ambapo amewapongeza wadau hao kwa kuwa na maono yanayounga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza sekta ya Mifugo.
Akiwa kwenye kiwanda cha Kilimanjaro Dkt. Madele amesema kuwa kiwanda hicho mbali na kuwa fursa ya kuwahamasisha wafugaji kuzalisha maziwa kwa wingi kimetekeleza kwa vitendo sehemu ya vipengele vilivyopo kwenye mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwakusanya wafugaji kwenye vikundi na kujenga vituo vya kukusanyia maziwa.
“Sisi kama Serikali kupitia mradi huo tumeanza kuongeza nguvu kwenye matumizi ya teknolojia ya uhimilishaji ili kuhakikisha wafugaji wetu wanapata ng’ombe wanaozalisha maziwa kwa wingi kwa sababu mpaka sasa pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye viwanda hivi bado asilimia kubwa vinazalisha chini ya nusu ya kiwango chake kilichosimikwa” Ameongeza Dkt. Madele.
Akiwa kwenye shamba la mwekezaji binafsi la kuzalisha malisho ya Mifugo na maziwa la Nuru lililopo Wilaya ya Arumeru,Dkt. Madele amempongeza mwekezaji huyo kwa kuwa na maono ya muda mrefu yanayoonesha namna alivyodhamiria kufanya mapinduzi kwenye ufugaji ambapo ameahidi kumsaidia kumuunganisha na Taasisi za fedha ili aweze kutekeleza azma yake.
“Changamoto kubwa inayokukabili hapa ni mtaji na mpaka sasa najiuliza mtu mwenye uwekezaji wa aina hii unawezaje kukosa mkopo wakati kuna watu wanapata mikopo wakiwa na “briefcase” tu mkononi, hili haliwezekani ntaenda kukaa na wataalam wetu tuone namna gani tunaweza kukufanikishia kupata mkopo unaohitaji” Amesisitiza Dkt. Madele.
Mbali na kutembelea wadau hao, Dkt. Madele pia alitembelea Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Tengeru ambapo alivutiwa na uwezo mkubwa wa mafunzo kwa vitendo walionao wanafunzi wa kampasi hiyo kisha akaelekea kwenye Kituo cha Taifa cha uhimilishaji (NAIC) ambako alifanya kikao na wataalam wa Taasisi hiyo na wahimilishaji waliopo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ili kujadili changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.





Maoni
Chapisha Maoni