DKT. MADELE ATETA NA WAFANYABIASHARA WA MIFUGO NAMANGA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Fabian Madele amekutana na wafanyabiashara wa Mifugo waliopo eneo la Namanga mkoani Arusha kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.
Dkt. Madele amekutana na wafanyabiashara hao Julai 20,2026 ambapo aliwapa fursa ya kuzungumza kero zinazowakabili na maoni waliyonayo katika kuboresha biashara ya Mifugo kwenye mnada huo ambapo waliiomba Wizara yake kutengeneza mazingira na sera wezeshi ili waweze kuuza mifugo yao kwenye mnada huo badala ya kwenda kuiuza nchini Kenya.
“Huu mnada ungeboreshwa na Sera nzuri ikatengenezwa, badala ya sisi kusafirisha mbuzi wetu kwenda Kenya, Wakenya wavutiwe kuja kuchukua mbuzi huku kwetu kwa makubaliano ambayo Serikali yetu na ya kwako watakubaliana ambapo itatusaidia kuokoa hasara ya usafirishaji na tutalipa mapato ya Serikali yetu” Amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Akijibu hoja hizo Dkt. Madele amesema kuwa atakaa na watalaam wake na kuzitafutia ufumbuzi huku akiahidi kukutana tena na wafanyabiashara hao ili kuwa na mjadala mpana zaidi wa kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazowakabili.
“Hii habari ya biashara ya kimataifa hatuwezi kuizuia lakini lazima ifanyike kwa maslahi ya pande zote mbili na sio kinyume chake lakini tunayo haja kama Serikali ya kuhakikisha hii biashara ya Mifugo inayofanyika kwenye mpaka huu imekaa vizuri na ifanyike kwa tija kwa mfugaji na Serikali yetu kama Taifa” Amesisitiza Dkt. Madele.
Aidha Dkt. Madele ametoa rai kwa wafanyabiashara hao kuwa wazalendo na kujiepusha na vitendo vya kutorosha mifugo ambapo amewaeleza kuwa mapato yanayopatikana hapa nchini yanawezesha upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii ikiwemo maji, elimu na ujenzi wa barabara.
Mpaka wa Namanga una urefu takribani km. 750 ambapo shughuli za minada ya Mifugo hufanyika kwenye eneo hilo huku wanunuzi wakubwa wa mifugo hiyo wakitokea nchi jirani ya Kenya.





Maoni
Chapisha Maoni