DKT. BASHIRU AZIKARIBISHA KAMPUNI KUTOKA ITALIA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa leo Juni 14, 2026 amekutana na ujumbe wa kampuni mbili kutoka nchini Italia ambayo ni ITARE na MULMIX katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Kambarage Tower jijini Dodoma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuangalia maeneo ya uwekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi.
Kampuni ya ITARE kutoka nchini Italia inajihusisha na ushauri wa kifedha yenye mchanganyiko wa kipekee wa utalaamu na uzoefu katika fedha za miradi na biashara pamoja na uendelezaji wa biashara katika masoko yanayoibukia, ikiwa na mkazo maalum katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kampuni ya MULMIX imejikita katika usanifu, uzalishaji na usimikaji wa vihenge na mitambo ya kuhifadhia nafaka katika sekta ya kilimo.
Baada ya ujumbe wa kampuni hizo kujitambulisha na kuonyesha utayari wa kuwekeza nchini Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amezihakikishia kampuni hizo kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuwekeza na kufanya biashara kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya mifugo na uvuvi kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi(PPP).
Aidha, Balozi Dkt. Bashiru ameyataja maeneo muhimu ya kuwekeza kwa sasa katika sekta hiyo kuwa ni uboreshaji wa kosafu za mifugo, uwekezaji katika vyakula vya mifugo na samaki, tasnia ya kuku, miundombinu na teknolojia ya uzalishaji na uchakataji wa maziwa na ukuzaji viumbe maji.






Maoni
Chapisha Maoni