DKT. BASHIRU AMALIZA MGOGORO WA WAFUGAJI WEST KILIMANJARO
◼️Awataka “Laigwanan” kusimamia maadili kwenye jamii yao
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amemaliza mgogoro wa wafugaji waliopo kwenye ranchi ya Mifugo ya West Kilimanjaro iliyopo Siha mkoani Kilimanjaro ambapo amewataka viongozi wa kimila wa kaya za kimasai maarufu kama “Laigwanan” kuendelea kuhimiza elimu ya maadili kwa kwenye jamii zao ili kukomesha vitendo vya kihalifu kwenye maeneo yao.
Balozi Dkt. Bashiru amefanikiwa kumaliza mgogoro huo uliokuwa ukihusisha mwekezaji na wafugaji wanaozunguka ranchi hiyo mara baada ya kufika hapo na kufanya kikao na pande zote zinazokinzana Julai 17,2026 ambapo amewasisitiza wafugaji hao kuwa mfugaji mkubwa na mdogo wote wapo sawa mbele ya sheria.
“Mimi siwezi kuwa Waziri nayetembea kwenye mashamba ya wawekezaji wakubwa wenye ng’ombe nzuri wanaotoa maziwa huku wafugaji wadogo ambao ndo wengi wakiwa wamechoka pamoja na ng’ombe wao na hapo Uwaziri wangu utakosa mashiko” amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Christopher Timbuka mbali na kumshukuri na kumpongeza Balozi Dkt. Bashiru kwa kufanikiwa kusimamia suluhu ya mgogoro huo amemuahidi kushirikiana na viongozi wa kimila wa kabila la wamasai kuhakikisha mgogoro wa aina hiyo hautokei tena.
“Migogoro hii hutokana na kutokuwa na uelewa mzuri wa namna ya kumaliza changamoto zinazojitokeza na sisi kwa upande wa Serikali ya Wilaya tutaendelea kushirikiana na Mhe. Mkuu wa mkoa katika kuhakikisha yale yote ambayo tumeyapokea kutoka kwako tunayatekeleza” Ameongeza Mhe. Timbuka.
Naye mwakilishi wa vijana wanaozunguka ranchi hiyo Bw. Emanuel Emanuel amesema kuwa wamejifunza kuwa panapotokea changamoto zozote za utatuzi wa migogoro wanapaswa kuwasikiliza viongozi wao wa kimila.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inakomesha migogoro kwa jamii zinazozunguka ranchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwakabidhi hekta 9000 ili wazitumie kwenye shughuli zo nyingine.



Maoni
Chapisha Maoni