BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI AFRIKA MASHARIKI LA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA LAKUTANA
Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limekutana jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuleta mageuzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha lishe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa 19 wa Baraza hilo uliofanyika Julai 2, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh, amesema wajumbe walijadili taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mikutano iliyopita, hali ya usalama wa chakula na lishe katika ukanda wa Afrika Mashariki, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Kilimo katika Bara la Afrika (CAADP).
Prof. Sheikh amesema Baraza hilo pia lilijadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha maendeleo ya sekta hizo, ikiwemo Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, afua za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mifumo ya kilimo na usalama wa chakula, maendeleo ya utekelezaji wa Mpango wa Hatua za Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula (EAC SPS Programme), uoanishaji wa viwango na taratibu za pembejeo za kilimo, pamoja na Mradi wa Kuwezesha na Kuimarisha Huduma za Ugani Endelevu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Prof. Sheikh amebainisha maeneo mengine ambayo wamejadili, ikiwemo Biashara za mipakani ya mazao ya chakula, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani kwa mazao hasa mpunga na Takwimu kwa mazao ya chakula, mifugo na samaki.
Vilevile, Prof. Sheikh amesema maamuzi yatakayotekelezwa kupitia mikakati hiyo yanatarajiwa kuongeza tija katika uzalishaji, kuimarisha biashara ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo wa 19 wa Baraza ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu pamoja na Kikao cha Wataalamu, vilivyofanyika kuanzia Juni 30 hadi Julai 1, 2026, kwa lengo la kupitia na kuandaa mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya maamuzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, sera na mipango kutoka nchi wanachama za Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.








Maoni
Chapisha Maoni