WANANCHI WAJITOKEZA KUJIFUNZA UFUGAJI BORA KATIKA BANDA LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

Wananchi mbalimbali wanaendelea kutembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho ya Mifugo na Mnada wa Kimataifa yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mbogo Ranchi, Ubena Zomozi, wilayani Chalinze mkoani Pwani, kwa lengo la kujifunza teknolojia na mbinu bora za ufugaji zinazolenga kuongeza tija na kukuza uchumi wa mifugo.

Wakiwa katika banda hilo, wananchi wanapata elimu kuhusu uzalishaji na uhifadhi wa malisho ya mifugo, umuhimu wa kupima ubora wa maziwa, teknolojia ya uhimilishaji, huduma za chanjo na udhibiti wa magonjwa ya mifugo, pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika sekta ya mifugo.

Aidha, wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na kujibu maswali ya wananchi ili kuwawezesha kufanya ufugaji wenye tija, unaozingatia matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kisasa.

Katika maonesho hayo yaliyoandaliwa na Mbogo Ranchi, taasisi mbalimbali za sekta ya mifugo zinashiriki kutoa huduma na elimu kwa wananchi, zikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Kampuni ya Taifa ya Uhimilishaji (NAIC).

Ushiriki wa taasisi hizo unalenga kuhakikisha wafugaji na wananchi kwa ujumla wanapata elimu, huduma na teknolojia zitakazowawezesha kuendesha ufugaji wenye tija na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Tembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ujifunze teknolojia na mbinu bora za ufugaji kwa maendeleo ya mifugo na uchumi wako.









Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO