SERIKALI YAONGEZA HAMASA YA UNYWAJI WA MAZIWA, WATOTO WAPEWA KIPAUMBELE
Serikali kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania imeendelea kuhamasisha matumizi ya maziwa nchini kwa kutoa elimu kwa wananchi, wanafunzi na wadau wa sekta kuhusu umuhimu wa maziwa katika kuboresha afya na lishe.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa paketi 2,110 za maziwa ya mililita 500 kwa wanafunzi wa shule sita za msingi mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya 29 ya Maziwa Kitaifa yanayoendelea kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya, alisema serikali imejipanga kuhakikisha Watanzania, hususan watoto, wanapata virutubisho muhimu vinavyopatikana katika maziwa kwa ajili ya ukuaji bora wa mwili na akili.
Prof. Msalya alisema watoto wamepewa kipaumbele katika mkakati wa kuongeza matumizi ya maziwa nchini kutokana na mahitaji yao makubwa ya virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa.
Aidha Prof. Msalya ameeleza kuwa serikali imeanza kutekeleza mpango wa kupeleka maziwa shuleni mara kwa mara ili kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutumia maziwa kama sehemu ya lishe ya kila siku.
“Serikali inaendelea kushirikiana na walimu, wazazi, kamati za shule na wadau wa elimu ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na watoto wanapata maziwa kwa manufaa ya afya zao,” alisema Prof. Msalya.
Katika hatua nyingine, alisema serikali kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi inapanga kuanzisha vituo maalumu vya unywaji wa maziwa, vinavyojulikana kama baa za maziwa, katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa vituo hivyo vitatoa aina mbalimbali za maziwa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi.
Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya maziwa katika ofisi za umma na sekta binafsi, ambapo baadhi ya taasisi tayari zimeanza kutoa maziwa kwa watumishi wake kama njia ya kuimarisha afya na kuongeza tija kazini.
Kuhusu uzalishaji wa maziwa, Prof. Msalya alisema serikali inalenga kuongeza uzalishaji kutoka lita bilioni 4.2 za sasa hadi zaidi ya lita bilioni 13 katika miaka ijayo. Alisema zaidi ya Sh bilioni 500 zimetengwa kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu, mifugo na maeneo mengine muhimu yatakayochochea ongezeko la uzalishaji.
Alisisitiza kuwa maziwa hayapaswi kutumiwa wakati wa ugonjwa pekee, bali yanapaswa kuwa sehemu ya lishe ya kila siku kwa watu wa rika zote ili kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa shule ya mahitaji maalumu, Reina Mgimwa, aliipongeza serikali kwa mpango wa ugawaji wa maziwa shuleni na kuomba uendelezwe kutokana na mchango wake katika kuboresha afya na maendeleo ya wanafunzi.
Maadhimisho, ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yanaendelea nchini yakiwa na lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa maziwa katika lishe, afya na maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.





Maoni
Chapisha Maoni