SERIKALI NA BROOKE EAST AFRICA KUIMARISHA USTAWI NA ULINZI WA PUNDA NCHINI
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kuimarisha mikakati na hatua mbalimbali zinazolenga kuboresha ustawi wa punda nchini, ikiwemo upatikanaji wa lishe bora, maji, huduma za afya, ulinzi pamoja na matumizia salama ya wanyama hao.
Akizungumza leo Juni 9, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao na Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Brooke East Africa, Dkt. Raphael Kinoti, pamoja na watendaji wa shirika hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha ustawi na usalama wa mifugo akiwemo punda unaendelea kuimarika kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya ustawi wa wanyama.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho ya sera, sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya mifugo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha mfumo wa sera na sheria zinazolinda mifugo ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta na kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa,” amesema Dkt. Bashiru.
Aidha, Waziri huyo amesema sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta za kimkakati zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia mnyororo mzima wa thamani wa mifugo na mazao yake, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha ustawi wa wanyama ili kuongeza tija na uzalishaji.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza programu na miradi inayolenga kulinda haki na ustawi wa wanyama, hususan punda ambao wana mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wengi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, amesema Wizara ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Brooke East Africa katika kuandaa mitaala na programu za mafunzo zitakazosaidia kuongeza uelewa kuhusu ustawi wa punda pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu ili kubaini idadi halisi ya punda nchini kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma.
Naye Mkurugenzi wa Kanda wa Brooke East Africa, Dkt. Raphael Kinoti, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikia katika kuimarisha ustawi wa punda, akieleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa
nchi zinazoongoza barani Afrika katika kuweka mifumo na miongozo ya matibabu na ustawi wa punda.
Amesema Brooke East Africa itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mazingira wezeshi ya kulinda ustawi wa punda na kuhakikisha wanyama hao wanapata huduma stahiki zinazowawezesha kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ufanisi zaidi.







Maoni
Chapisha Maoni