SERIKALI KUANDAA MWONGOZO WA ULINZI NA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI
Na. Stanley Brayton, WMUV
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kuandaa Mwongozo wa Utendaji Kazi kwa ajili ya Shughuli za Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi nchini ikiwa na lengo la kuandaa Mwongozo ambao utawezesha utekelezaji wa majukumu ya Usimamizi wa Rasilimali hizo kufanyika kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotumika katika Sekta ya Uvuvi.
Akizungumza leo Juni 11, 2026 Mkoani Morogoro, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uvuvi Nchini, katika Kikao kazi cha Kuandaa Mwongozo huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Christian Nzowa amesema kuwa Wizara imekutana na wadau mbalimbali kutoka Halmashauri zenye Maeneo ya Uvuvi wa mwambao wa Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa, Maji Madogo na Bahari ya Hindi, pamoja na Maafisa Wandamizi Wastaafu wa Uvuvi na Maafisa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili kupitia Mwongozo wa kiutendaji ujulikanao kama Standard Operating Procedure SOPs, na ambao utatumika kudhibiti Uvuvi haramu
"Ili Kanuni itekelezeke lazima tuwe na Mwongozo ambao unaendana na Dira ya Taifa ya Mwaka 2050, na ambao utatumika kwa Maafisa Doria wote nchini pamoja Maafisa wanaoshughulika na ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi" amesema Ndg. Nzowa
Aidha, Ndg. Nzowa amesema Mwongozo huo utatumika kwa Tanzania Bara pekee, na utajumuisha maeneo Makuu matatu, ambapo eneo la kwanza litaonesha jinsi ya kufanya Doria Ziwani au Baharini, eneo la pili litaonesha ni kwa jinsi gani Doria ya nchi kavu inavyofanyika ikiwa ni pamoja na Viwanda na maghala yote ya bidhaa za Uvuvi, na eneo la tatu ni jinsi ya kufanya Doria katika maeneo ya anga.
Vilevile, Ndg. Nzowa, amesema kuwa Mwongozo huo utakuwa msaada tosha katika kutekeleza Kanuni za Uvuvi, na utaandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, na kabla ya kuanza kutumika utapelekwa kwa wadau mbalimbali ili wauchambue na kuukubali.
Pia, Ndg. Nzowa ameweka wazi kuwa lengo la Mwongozo huo si kulinda Mazao ya Uvuvi tu bali kuhakikisha Uzalishaji wa Mazao hayo yanaongezeka, kwani Mazao ya Uvuvi yamepungua sana kutokana na Uvuvi haramu.





Maoni
Chapisha Maoni