RIDHIWANI AVUTIWA NA HUDUMA ZINAZOTOLEWA BANDA LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Na. Chiku Makwai- Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete ameonesha kuvutiwa na huduma na elimu mbalimbali zinazotolewa katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi alipotembelea banda hilo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo, Waziri huyo alipata maelezo kutoka kwa wataalamu wa Wizara na taasisi zake kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi, ikiwemo ushauri wa kitaalamu katika sekta za mifugo na uvuvi, fursa za uwekezaji, pamoja na mikakati inayotekelezwa na Serikali katika kuendeleza sekta hizo kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.
Waziri Ridhiwani alieleza kuridhishwa na namna wataalamu wanavyotoa huduma kwa wananchi kwa ukaribu na ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kutumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kusikiliza changamoto zao ili kuboresha utoaji wa huduma.
Aidha, alisifu juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya teknolojia na mbinu bora za ufugaji na uvuvi, akibainisha kuwa hatua hiyo inachangia kuongeza tija, ajira na kipato kwa wananchi wanaojishughulisha na sekta hizo.
Kwa upande wao, wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameendelea kuwahudumia wananchi wanaotembelea banda hilo kwa kutoa elimu, ushauri na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya sekta hizo, Wananchi wamehimizwa kuendelea kutembelea banda la Wizara ili kunufaika na huduma zinazotolewa katika kipindi chote cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026.


Maoni
Chapisha Maoni