MIPANGO MAHSUSI IKIWEMO YA TASFAM YATAJWA KUONGEZA THAMANI YA PWEZA
Na. Edward Kondela
Wadau wa uvuvi waja na mipango mahsusi ya kuongeza thamani ya samaki aina ya pweza ukiwemo wa kuboresha miundombinu ya masoko na maeneo ya kushushia samaki hao, kupitia Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa Bahari Tanzania (TASFAM).
Akizungumza (28.05.2026) jijini Dar es Salaam, wakati wa kufungua kikao cha siku mbili cha wadau hao kutoka katika halmashauri za Ukanda wa Pwani zinazovua pweza, Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Christian Nzowa amesema changamoto kubwa kwa sasa ni upotevu wa mazao hayo baada ya kuvuliwa hususan nyakati za mvua na mavuvi yanapokuwa mengi.
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi. Agnes Meena, Bw. Nzowa amesema kwa sasa miundombinu ya barafu na kuhifadhia pweza bado haijakaa vizuri, hivyo kupitia mradi wa TASFAM ambao umejikita kuboresha sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani, baadhi ya miundombinu hiyo itaboreshwa hivyo kuongeza thamani ya samaki hao ambapo kwa siku zinavuliwa tani 15 hadi 20 msimu unapokuwa mzuri baada ya kufungua miamba ya pweza.
“Ükanda wa Pwani kuna maeneo makubwa ya uvuvi wa samaki aina ya pweza, maeneo hayo kwa siku wanavua tani nne hadi tano kipindi cha msimu ambao siyo mzuri, lakini msimu unapokuwa mzuri wanavuna tani 15 hadi 20, mara nyingi samaki hawa husafirishwa kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchakatwa viwandani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi, katika nchi za Ulaya na Asia.” amefafanua Bw. Nzowa
Aidha, amebainisha kuwa katika kikao cha siku mbili wadau wanapitia mpango wa kusimamia samaki aina ya pweza ambao tayari umeshaandaliwa na wataalamu hivyo kutoa wigo kwa wadau hao wakiwemo kutoka halmashauri za mikoa ya Ukanda wa Pwani ambapo samaki aina ya pweza huvuliwa ili kuupitia na kuuboresha.
Pia, ametoa wito kwa wananchi wa maeneo ya Ukanda wa Pwani ambapo samaki aina ya pweza wanapatikana, waendeleze utaratibu wa kufunga na kufungua miamba ya pweza kwa kuwa inaongeza kipato kwao wenyewe, kuongeza chakula pamoja na ushirikishaji katika jamii yao kwenye suala zima la afya bora na kuzikumbusha halmashauri zote ambazo zinavua pweza kusimamia majukumu ya msingi ya ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kudhibiti utoroshaji wa mazao hayo.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mratibu wa mavuno ya pweza Bw. Melkizedeck Koddy, amesema kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kila aina ya uvuvi lazima uwe na mpango mahsusi wa usimamizi kwa sababu uvuvi unatofautiana kulingana na aina ya samaki hata kama mazingira yanafanana, nyenzo zinazotumika ni tofauti kwa hiyo kunapokuwa na mpango wa usimamizi unasaidia katika kutengeneza usimamizi bora na endelevu.
Ameongeza kuwa, mazao ya uvuvi ynayokwenda nje ya nchi kutoka Ukanda wa Pwani kwa msingi wa uthamani, pweza wanaongoza kwani uvunaji wake unafikia tani laki saba hadi nane kwa mwaka na mitaani wanaongoza kwa thamani, hivyo kuna mahitaji makubwa ya pweza lazima kuwepo usimamizi shirikishi na endelevu, unaohusisha jamii ili kuwa na mpango utakaokidhi haja ya usimamizi endelevu.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho, wamesema uhitaji wa pweza ni mkubwa ukilinganisha na upatikanaji wake hususan kwenye masoko ya nje ya nchi, hivyo wanatumaini njia ya kufunga miamba ya pweza kwa miezi mitatu mitatu ni muhimu ili kuzaliana na kufikia uzito unaotakiwa katika soko.
Wamesema njia hiyo imekuwa ikisaidia kuona pweza wachanga wanakuwa na wengine kuhamia kwenye miamba iliyofungwa kwa kuwa wanapenda kuwa sehemu salama, hivyo kupata mazao mengi wakati wa kufungua miamba.
Madhumuni ya kikao hicho ni kujadiliana na wadau kupitia mpango wa usimamizi na kutoa maoni yao kwa mujibu wa uzoefu ili kuhakikisha uvuvi wa pweza unakuwa endelevu na rafiki kwa mazingira wanayotoka.


Maoni
Chapisha Maoni