MASAUNI AITAKA JAMII KUTUNZA MAZINGIRA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameitaka jamii kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Masauni ametoa wito huo leo Juni 4, 2026, alipotembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
Akizungumza Katika Maonesho hayo, Mhe. Masauni amesema Tanzania inaendelea kukabiliwa na changamoto za mabadliko ya tabianchi zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira, hivyo akasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhifadhi mazingira.
“Tunajua kuwa kama nchi tuna changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanayotokana na uharibifu wa mazingira. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zilizopo hapa tunafanya juhudi kubwa kulitatua tatizo hili. Nizipongeze sana taasisi hizi kwani yote waliyoonesha hapa yanalenga kuhifadhi na kutunza mazingira,” amesema Mhe. Masauni.
Ameeleza kuwa maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha ubunifu, teknolojia na mikakati mbalimbali inayolenga uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Maadhimisho ya wiki ya Mazingira Kitaifa yalianza Juni 1, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa kesho Juni 5, 2026, ambapo mgeni rasmi katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Dkt. Emmanuel Nchimb, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho hayo yanaendelea kufanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “DIRA 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

Maoni
Chapisha Maoni