MAJOSHO 754 YAJENGWA KUOGESHEA MIFUGO NCHINI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema itaendelea kuratibu ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa miundombinu muhimu ya mifugo nchini, ikiwemo majosho katika Wilaya ya Bunda, kwa lengo la kuimarisha huduma za mifugo na kudhibiti magonjwa yanayoathiri mifugo kadri ya upatikanaji wa fedha.

Kauli hiyo imetolewa leo June 2,2026 bungeni na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt Bashiru Ally Kakurwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere,(CCM)  aliyehoji ni lini Serikali itajenga majosho katika maeneo ya wafugaji ya Mahanga, Tingirime, Nyabuvumbu, Nyabuzume, Kaloreli na Tirig’ati.

Akijibu Balozi Dkt. Bashiru alisema Serikali inatambua umuhimu wa majosho katika kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe na mbung’o, na kwamba tangu mwaka wa fedha 2021/2022 imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa majosho ambapo hadi sasa jumla ya majosho 754 yamejengwa nchini kote.

Alisema  kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitumia shilingi milioni 92 kujenga majosho manne katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwenye vijiji vya Chingulubila, Mwitende, Salama na Mariwanda, ambayo yote yamekamilika kwa asilimia 100 na yanaendelea kutoa huduma kwa wafugaji.

Aidha, Balozi Dkt. Bashiru  alitoa rai kwa halmashauri nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya majosho ili kuimarisha afya ya mifugo, kudhibiti magonjwa na kuongeza tija katika sekta ya mifugo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO