DKT. MWIGULU ATAKA KILIMO CHA MALISHO KUWA MWAROBAINI WA MIGOGORO YA WAFUGAJI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wafugaji kulima malisho ya mifugo ili kupunguza changamoto ya migogoro ya ardhi na ukosefu wa malisho ya mifugo.

Mhe. Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Juni 19, 2026 Wilayani Chalinze Mkoani Pwani wakati akifungua Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo na kueleza kuwa changamoto  ya uhaba wa malisho imekuwa kikwazo  kwa wafugaji nchini, hivyo amewahimiza wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo kutumia maonesho hayo kujifunza juu ya kilimo cha malisho, uboreshaji wa mbegu za mifugo ili kuleta tija na kuchangia pato la taifa.

“Nitumie fursa hii kuwahimiza wadau wote wa mifugo nchini kutumia fursa ya maonesho haya kujifunza kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji na kilimo cha malisho ya mifugo ili kuongeza uzalishaji, kuuza na kununua mifugo bora kwenye minada inayoambatana na maonesho haya." amesema Mhe. Dkt. Mwigulu 

Aidha, Mhe. Dkt. Mwigulu ameielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kushirikiana na wafugaji katika kutekeleza Kampeni ya kuzalisha malisho kwa kuwapatia elimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuiagiza Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutenga na kusimamia maeneo ya malisho ili kuwa na matumizi bora ya ardhi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameelezea lengo kuu la maonesho hayo ni kujenga Mfumo imara wa biashara ya mifugo na mazao yake kwa kuwakutanisha wafugaji, wafanyabiashara na wadau wote katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya mifugo ili kubadilishana uzoefu,  kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji pamoja na kupanua fursa za masoko nchini na katika mataifa mengine. 

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema Wizara inaendelea na mikakati kuzalisha mbegu za malisho katika mashamba ya Serikali na mashamba  ya binafsi na kuhamasisha kwa kutoa elimu kwa wafugaji juu ya kilimo cha malisho ili kuboresha lishe ya mifugo, kuimarisha upatikanaji wa chakula cha mifugo kupunguza au kuondoa kabisa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena amesema Maonesho hayo na Mnada wa Mifugo ambayo yameandaliwa na Ranchi ya Mbogo ni ishara tosha kuwa Serikali inashirikiana vyema na Sekta Binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta katika kufanya mageuzi ya Sekta na kuongeza uzalishaji nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge amesema Mkoa wa Pwani umendelea sana katika kufanya Mageuzi katika Sekta ya Mifugo, ambapo mpaka sasa Mkoa umeshaanda Ranchi 921 za Mifugo kwa ajili ya wafugaji, na imeshatoa hati za kimila 419 kwa wafugaji ili waweze kufuga kisasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ranchi ya Mbogo, Bw. Naweed Mulla ameelezea changamoto mbalimbali zinazowakumba wafugaji, ikiwemo ukosefu wa vinasaba bora, Malisho, Magonjwa ya Mifugo na Masoko, na ameiomba Serikali iweke Mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kujishughulisha na Masuala ya Mifugo ili kukuza Uchumi wao na Pato la Taifa kiujumla.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (DGLF), Dkt. Asimwe Rwiguza (wa pili kulia), akimuonesha na kumuelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kushoto), Malisho ya aina mbalimbali ambayo yanatumika kulisha Mifugo, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani, wa tatu kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akihutubia wadau wa Sekta ya Mifugo, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na wadau wa Sekta ya Mifugo, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kushoto), akisalimiana na Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (DGLF), Dkt. Asimwe Rwiguza (wa nne kushoto), akimuelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa tatu kushoto), Teknolojia mbalimbali za upandaji Malisho, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani, wa kwanza kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa tatu kulia), akimuelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa nne kulia), namna ya kuhifadhi Malisho ya Mifugo, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa tatu kulia), akizungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa kwanza kushoto) kuhusiana na utatuzi wa Malisho ya Mifugo, katika Uzinduzi wa Maonesho na Mnada wa Mifugo, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Juni 19, 2026, Chalinze - Pwani.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO