DKT. MHINA AHIMIZA USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI KATIKA KUIMARISHA MATUMIZI YA CHANJO ZA MIFUGO
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina, amesema kuwa matumizi sahihi ya chanjo ni moja ya nyenzo muhimu katika kudhibiti magonjwa ya mifugo, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa sekta ya mifugo nchini.
Dkt. Mhina ameyasema hayo leo Juni 16, 2026 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo kuhusu Chanjo na Uchanjaji wa Mifugo ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, GALVmed, FAO Tanzania na TAHO.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Mhina amesema sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania kupitia usalama wa chakula na lishe, ajira, kipato cha kaya pamoja na mauzo ya bidhaa za mifugo ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, amesema maendeleo ya sekta hiyo bado yanakabiliwa na changamoto za magonjwa mbalimbali ya mifugo yakiwemo Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR), Ugonjwa wa Midomo na Miguu (FMD), Brucellosis na Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP), ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa matumizi sahihi ya chanjo na kuimarisha biosecurity.
"Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya ya wanyama ikiwemo maboresho ya sera, kuimarisha huduma za mifugo, ufuatiliaji wa magonjwa na utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo.
Aidha, Dkt. Mhina amesema kupitia kampeni ya kitaifa ya chanjo iliyoanza mwaka 2025/2026, Serikali imekusudia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 216 katika kipindi cha miaka mitano kudhibiti magonjwa ya kipaumbele na kuboresha huduma za chanjo katika mamlaka za serikali za mitaa nchini." Amesema Dkt. Mhina
Pia, Dkt. Mhina amesisitiza kuwa kaulimbiu ya mkutano huo inayosema “Kuongeza Matumizi ya Chanjo kwa Mifugo kwa Afya na Uzalishaji Endelevu wa Mifugo kupitia Ushiriki wa Sekta Binafsi” inaakisi umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, watengenezaji wa chanjo, wasambazaji, wataalamu wa mifugo, vyama vya wafugaji na washirika wa maendeleo katika kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa urahisi na zinawafikia wafugaji wote nchini.
Vilevile, Dkt. Mhina amezindua rasmi awamu ya pili ya Mradi wa VETERINARY INNOVATION TRANSFORMING ANIMAL HEALTH AND LIVELIHOOD (VITAL 2) unaotekelezwa na GALVmed, unaolenga kuimarisha upatikanaji, usambazaji na matumizi ya chanjo za mifugo nchini. Uzinduzi huo unaonyesha dhamira ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuendelea kuwekeza kwenye afya ya mifugo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha ya wafugaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Maoni
Chapisha Maoni