DKT. MDETELE AELEZEA MPANGO MKAKATI WA SERIKALI KUTOKOMEZA MAGONJWA YA MIFUGO KIKAO CHA ADB
◾Aelezea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania katika Huduma za Mifugo ikiwemo Udhibiti wa Magonjwa na Utambuzi wa Mifugo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Magonjwa ya Mlipuko na magonjwa yasiyo na Mipaka (E&TADs), Dkt. Daniel Mdetele ameelezea Mpango Mkakati wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutokomeza Magonjwa ya Mifugo ili kuongeza uzalishaji wa Mifugo yenye ubora zaidi ikianzia kwa Mifugo yenyewe hadi Mazao yake.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), uliofanyika leo Mei 28, 2026 nchini Jamuhuri ya Congo (Congo Brazzaville), Dkt. Mdetele ameelezea jinsi uwekezaji huo mkubwa ulivyofanywa na Serikali ya Tanzania katika Huduma za Mifugo kupitia Mpango wa Kitaifa wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Magonjwa na Utambuzi wa Mifugo wenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 85.
“Mwaka 2025/2026, jumla ya Dola Milioni 24 zimeshatolewa kugharamia Chanjo, Vifaa vya Utambuzi, Vifaa vya TEHAMA, Pikipiki na Malipo ya wachanjaji uwandani.” amesema Dkt. Mdetele
Aidha, Dkt. Mdetele ameeleza kuwa katika Mwaka 2026/2027, Serikali imetenga jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 13 kwa lengo la kuendeleza Kampeni hiyo ya Kitaifa ya Chanjo za Mifugo, inayolenga kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) ifikapo Mwaka 2030.
Vilevile, Dkt. Mdetele ameziomba Taasisi za Kikanda na Kimataifa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchukuaji wa hatua za uwekezaji kwenye eneo la Afya za Wanyama kwa lengo la kuwezesha biashara salama ya Mifugo na mazao yake, usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magonjwa yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu hususan Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa.

Maoni
Chapisha Maoni