DKT. BASHIRU AZINDUA MAADHIMISHO YA KITAIFA WIKI YA MAZIWA 2026

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa leo Mei 31,2026 amezindua Maadhimisho ya 29 ya kitaifa ya wiki ya Maziwa ambayo mwaka huu yanafanyika kwenye viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa Maadhimisho hayo yamekuwa na lengo la kuhamasisha uwekezaji, urasimishaji wa tasnia ya maziwa,matumizi ya maziwa bora na salama ili kulinda afya ya mlaji, kukuza biashara rasmi ya maziwa na kuhakikisha tasnia hiyo inaongeza mchango wake kwenye maendeleo ya kaya za wafugaji na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

“Sisi kama wizara kwa dhati kabisa kupitia mradi wetu wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadililo ya tabia nchi tutahakikisha mfugaji anajikwamua kiuchumi kwa sababu mradi huu umekusudiwa kununua na kufuga ng’ombe bora wa maziwa, kufanya ujenzi wa miundombinu itakayowezesha ufugaji bora, kuongeza uzalishaji na kuboresha mnyororo wa thamani wa maziwa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kukusanyia maziwa, kupanua soko la maziwa na kuanzisha bima ya mifugo” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru ametoa rai kwa wadau wote kuhakikisha uzalishaji wa maziwa kutoka lita Bil. 4 zinazozalishwa hivi sasa hadi lita Bil.8 huku akiwasisitiza kuhakikisha maziwa yanahifadhiwa na kusafirishwa kwa viwango vinavyokubaliwa.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya amewataka wananchi kutodharau matumizi ya maziwa na  kuondokana na dhana ya kufananisha maziwa na mazao mbalimbali.

“Wapo watu siku hizi wanaita maziwa ya nyuki na wengine wanaita maziwa ya soya ni lazima tuelewane kisayansi kuwa yale sio maziwa bali mbadala wake kwa sababu maziwa ni kimiminika kinachozalishwa na wanyama wanaonyonyesha hivyo hatuwezi kupata maziwa kutoka kwenye mimea au nyuki” Amesisitiza Prof. Msalya.

Maadhimisho hayo ya kitaifa ya Wiki ya Maziwa ambayo kwa mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Rasimisha Biashara ya Maziwa, Okoa Maisha ya Walaji, Ongeza Kipato, Changia Uchumi” yanatarajiwa kufika kilele chake Juni 1,2026 kupitia kongamano la wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa tasnia hiyo.

Mkurugenzi msaidizi hakimiliki za waboreshaji mbari na maendeleo ya kosaafu za wanyama Bw. Jeremiah Temu (kushoto) akimuelezea Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) namna kifaa maalum cha kuhifadhia mbegu za uhimilishaji kinavyofanya kazi yake wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya Maziwa mkoani Iringa Mei 31,2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kulia) akifafanua namna mfumo wa “Maziwa Hub” unavyoweza kutumika kuhamasisha matumizi ya Maziwa  muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Bodi ya Maziwa kabla ya kuzindua Maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya Maziwa mkoani Iringa Mei 31,2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akimkabidhi cheti cha pongezi mratibu wa Mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabia nchi Dkt.Lazaro Kapella kutokana na mchango wa uliotolewa na mradi huo kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya maziwa yanayoendelea mkoani Iringa Mei 31,2026.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO