DKT. BASHIRU AKOSHWA UWEKEZAJI SEKTA YA MAZIWA IRINGA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na kamati  ya kudumu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo  wamekoshwa na kiwango cha uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya Maziwa mkoani Iringa.

Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za ufugaji na uzalishaji maziwa kwenye kiwanda cha ASAS, Balozi Dkt. Bashiru amewataka wafugaji kuheshimu misingi ya sayansi na taaluma ili wawe na ufugaji wenye ufanisi na wa kibiashara.

“Tumeona wataalam ambao amewaajiri ASAS wanaelewa kazi yao na katika hili nchi imefundisha sana wataalam hivyo ni lazima tuheshimu utaalam wao lakini pia tuwape nafasi na nyenzo za kuonesha utaalam wao” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amempongeza mwekezaji huyo kwa kuweka miundombinu bora ya uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya ardhi kwa upande wa uzalishaji wa malisho ya mifugo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Serikali kwa wafugaji ili kuwa na uhakika wa chakula na maji ya kunyweshea mifugo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika amesema kuwa uwekezaji huo umeipa nguvu kamati hiyo ya kuishauri Serikali juu ya njia bora za kuendeleza sekta hiyo ya maziwa.

“Huu ndo uwekezaji ambao Watanzania tunautegemea kwa sababu tuna ardhi kama nchi lakini sidhani kama tumeitumia kama ambavyo ASAS wanaitumia, yaan kama tungekuwa na kampuni hata 10 tu kama hii tungekuwa mbali sana” Ameongeza Mhe. Mwanyika.

Naye Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Fuad Jaffer mbali na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa anaopewa ameongeza mbali na kuzalisha maziwa mkakati mwingine wa shamba hilo ni kuzalisha mitamba ili kuwasaidia wafugaji wengine wanaohitaji mbegu bora za ng’ombe wa maziwa.

Ziara hiyo iliendelea katika shamba la Mifugo na kiwanda cha kusindika maziwa cha Shafa huku kivutio kingine kwa viongozi hao kikiwa ni Shamba la mwekezaji Richard Philips maarufu kama Kibebe ambaye aliishukuru Serikali kwa kuwapatia chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa tatu kutoka kushoto mbele) akisikiliza maelezo juu ya namna ya kutengeneza robota kubwa la malisho ya mifugo maarufu kama “Hei” kutoka kwa  mtaalam wa shamba la kuzalisha maziwa la kampuni ya ASAS Bw. Wayne Swart wakati wa ziara yake shambani hapo na kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mei 30,2026 mkoani Iringa. Katikati ni Msajili wa Bodi ya Maziwa Prof. George Msalya na wa tatu kutoka kulia ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Fuad Jaffer.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akieleza yale aliyoyaona kwenye shamba la kuzalisha maziwa la kampuni ya ASAS mara baada ya kuhitimisha ziara yake shambani hapo Mei 30,2026 mkoani Iringa. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika na kushoto Mkurugenzi wa Shamba hilo Bw. Fuad Jaffer. Wengine pichani ni wajumbe wa kamati hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni ya kusindika maziwa ya ASAS Bw. Fuad Jaffer (kulia) akimkabidhi zawadi ya boksi la maziwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati wa ziara ya Dkt. Bashiru kiwandani hapo Mei 30,2026.

Mkurugenzi wa kampuni ya kusindika maziwa ya ASAS Bw. Fuad Jaffer (kulia) akimkabidhi zawadi ya boksi la maziwa Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakati wa ziara kamati hiyo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kiwandani hapo Mei 30,2026.

Mmiliki wa shamba la Mifugo la Kibebe Bw. Richard Philips akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo aina ya ng’ombe alionao shambani kwake muda mfupi baada ya kumtembelea shambani kwake eneo la Kibebe mkoani Iringa Mei 30,2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo na baadhi ya watendaji wa Wizara yake mara baada ya kumaliza ziara yao kwenye shamba la Mifugo la Kibebe mkoani Iringa Mei 30,3026.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO