BI. MEENA AWAASA WAFUGAJI KUJIFUNZA TEKNOLOJIA MBALIMBALI ZA UFUGAJI WA KISASA
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amewaasa Wafugaji kujifunza teknolojia mbalimbali za ufugaji wa kisasa ili kufuga kisasa na kwa tija zaidi.
Akizungumza leo Mei 30, 2026 Mkoani Shinyanga, katika Maonesho ya Mifugo ya Kanda ya Ziwa yajulikanayo kama Lake Zone Livestock expo 2026 nyenye Kauli mbiu ya Tufuge Kibiashara ambayo yameandaliwa na Kampuni ya FARMFLEX Group, Bi. Meena amesema Maonesho hayo ni fursa kwa wafugaji katika kujifunza na kupata elimu kuhusu teknolojia mbalimbali za ufugaji ili kuepukana na ufugaji wa kizamani na kujikita katika ufugaji wa kisasa wenye tija na wa kibiashara.
"Sisi tunaamini mifugo ni biashara, mifugo ni migodi na mifugo ni utajiri, na ndio mana tunawataka wafugaji wetu wajifunze kufuga kisasa ili kuongeza tija, ili kuhakikisha Sekta ya Mifugo inaongeza ajira, kipato cha wafugaji na mchango wake katika uchumi wa nchi." amesema Bi. Meena
Aidha, Bi. Meena ameweka wazi jinsi Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inavyoendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara ili Sekta binafsi ziweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuimarisha masoko, kuanzisha viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo pamoja na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.
Vilevile, Bi. Meena ametoa shukrani za dhati kwa Kampuni ya FARMFLEX Group kwa kujenga Kituo cha Umahiri kwa ajili ya kutoa elimu, ushauri na uwezeshaji wa wafugaji kuhusu namna ya kuendesha ufugaji wenye tija na kibiashara, ambapo maono yao yanaendana kabisa na Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali hususan Mpango wa Mabadiliko ya sekta ya Mifugo wa mwaka 2022/23-2026/27 wenye lengo la kuimarisha sekta ya mifugo ili kuongeza tija.
Pia, Bi. Meena, amesema Serikali inatambua mchango wa Sekta binafsi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini hususan kwa ushiriki wao katika kuinua sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya Mifugo, ambapo ina jidhihirisha katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inatambua ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kama msingi muhimu wa kujenga uchumi shindani na jumuishi, na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaamini kuwa maendeleo ya sekta ya mifugo hayawezi kufikiwa kwa nguvu za Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano madhubuti kati ya Serikali, sekta binafsi hususani vijana, taasisi za fedha na, watafiti.







Maoni
Chapisha Maoni