BI. MEENA ATAKA UTAFITI KUWA CHACHU YA MAENDELEO YA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena, amesema kuwa utafiti una nafasi kubwa katika kuleta mageuzi na maendeleo endelevu ya sekta za mifugo, uvuvi na ukuzaji viumbe maji nchini, hivyo ni muhimu kuhakikisha agenda za utafiti zinaendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Taifa.

Bi. Meena amesema hayo leo Juni 9, 2026, wakati akifungua Warsha ya Wadau ya Kupitia Ajenda za Taifa za Utafiti wa Mifugo pamoja na Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji za mwaka 2026–2030 iliyofanyika katika Ukumbi wa Brand Hotel jijini Dodoma.

Amesema uwepo wa wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, mashirika ya maendeleo, mamlaka za serikali za mitaa na wadau wengine wa sekta hizo unaonesha dhamira ya pamoja ya kutambua mchango wa utafiti katika kukuza uchumi wa Taifa.

"Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuimarisha shughuli za utafiti kwa kuanzisha taasisi maalumu za utafiti ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), zenye jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendesha tafiti za kisayansi katika sekta hizo." Amesema Bi. Meena

Amesema vipaumbele vya utafiti katika sekta za mifugo na uvuvi vimelenga kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa mazao kupitia mbari bora za mifugo na samaki, kudhibiti magonjwa, kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali na kuongeza kipato cha wafugaji pamoja na wavuvi nchini.

Aidha, Bi. Meena amebainisha kuwa ajenda zilizokuwa zikitumika zilifikia mwisho wa utekelezaji mwaka 2025, hivyo kuna umuhimu wa kuzifanyia mapitio ili ziendane na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kimazingira yanayoendelea kutokea duniani.

Hata hivyo amezitaka timu za wataalamu kuhakikisha ajenda mpya zinazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na vipaumbele vya Serikali kwa lengo la kuondoa umaskini na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti Mafunzo na Ugani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samweli . Mdachi ameeleza mchakato wa kuandaa ajenda hizo ambazo zinalenga kuongoza utekelezaji wa tafiti zenye tija Kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena, akizungumza na Wataalamu na wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi wakati wa kikao kazi cha kupitia Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo 2026–2030 na Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuaji Viumbe Maji 2026–2030, kilichofanyika katika ukumbi wa Brand Hotel, jijini Dodoma, Juni 9, 2026. Bi. Meena alisisitiza umuhimu wa utafiti katika kuimarisha tija, ushindani na maendeleo endelevu ya sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Bw. Samweli  Mdachi( aliyesimama),  akitoa utangulizi kwa Wataalamu na wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi wakati wa kikao kazi cha kupitia Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo na Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuaji Viumbe Maji za mwaka 2026–2030, kilichofanyika Brand Hotel, jijini Dodoma, Juni 9, 2026.

Mkurugenzi wa Utafiti kutoka TALIRI, Dkt. Andrew Chota( aliyesimama ),akitoa salamu za Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti wakati wa kikao kazi cha kupitia Ajenda za Taifa za Utafiti wa Mifugo na Uvuvi za mwaka 2026–2030, kilichofanyika Brand Hotel, jijini Dodoma, Juni 9, 2026.

Wataalamu na wadau wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao kazi Cha kupitia Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo 2026_2030 na Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji 2026_2030, kilichofanyika Katika Ukumbi wa Brand Hotel, jijini Dodoma Juni 9, 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena (aliyekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na kamati ya  wataalamu na wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi( Technical Team), walioshiriki kikao kazi cha kupitia Ajenda za Taifa za Utafiti wa Mifugo na Uvuvi za mwaka 2026–2030, kilichofanyika Brand Hotel jijini Dodoma, Juni 9, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO