BI. MEENA AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA SOKO LA SAMAKI KIPUMBWI KWA WAKATI

◾Mradi wafikia asilimia 60 za utekelezaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya World Class Engineering Contractors Limited kuongeza kasi ya ujenzi wa Soko la Samaki la Kipumbwi, lililopo Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa Wavuvi na wadau wa Sekta.

Akizungumza leo Juni 27, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Masoko ya Samaki Mkoani Tanga, Bi. Meena amesema Soko la Samaki la Kipumbwi ni miundombinu muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Uvuvi, kwani litawawezesha wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kuongeza thamani ya bidhaa zao, kukuza biashara na kuinua vipato vyao, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Amesema pamoja na umuhimu wa mradi huo, utekelezaji wake umefikia asilimia 60 pekee, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2026.

"Fedha zote za mradi zipo tayari, hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na soko hili kwa kuuza mazao yao ya uvuvi," amesema Bi. Meena.

Aidha, Bi. Meena amesema kwa sasa hawezi kutangaza muda wa nyongeza kwa mkandarasi, bali ameagiza wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya kikao na mkandarasi ili kuandaa mpango kazi wa kina utakaoainisha hatua za kuhakikisha mradi unakamilika kwa haraka.

Bi. Meena pia amesisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wafanyakazi katika eneo la mradi, akieleza kuwa nguvu kazi iliyopo kwa sasa haitoshi kukamilisha ujenzi ndani ya muda unaohitajika.

Amefafanua kuwa Mradi wa Soko la Samaki la Kipumbwi unatekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo la Kimataifa (IFAD).

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Miundombinu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Laula Cleophace, amesema wamepokea maelekezo ya Katibu Mkuu na wataendelea kushirikiana kwa karibu na mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unakamilika kwa wakati.

Naye, Mkandarasi wa Kampuni ya World Class Engineering Contractors Limited, Mhandisi Abdul Mustapha, amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu na wamejipanga kuongeza nguvu kazi pamoja na kuimarisha usimamizi wa shughuli za ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, akizungumza na Mkandarasi wa Kampuni ya World Class Engineering Contractors Limited na wataalam wa Serikali kuhusiana na Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Kipumbwi, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Pangani, Juni 27, 2026 Tanga.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohamed Sheikh (wa pili kushoto), akitoa mapendekezo yake kuhusiana na Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Kipumbwi, wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Wilayani Pangani, Juni 27, 2026 Tanga.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena (wa tano kulia), akikagua Miundombinu ya Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Kipumbwi, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Pangani, Juni 27, 2026 Tanga.

Picha ni muonekano wa Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Kipumbwi, uliopo Wilayani Pangani, Juni 27, 2026 Tanga.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI