WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA EQUITY BENKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amekutana na Watendaji Wakuu wa Benki ya Equity, na kufanya nao mazungumzo ambayo yalilenga kuboresha na kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha Wafugaji na Wavuvi kupata mikopo kwa urahisi zaidi.

Akizungumza leo Aprili 23, 2026 Jijini Dodoma katika Kikao cha kuimarisha mashirikiano hayo ili kukuza Sekta hizo, kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo Kambarage Towel, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru, amesema Wizara kwa sasa inaendelea kukutana na wadau mbalimbali wa Sekta za Mifugo na Uvuvi ili kuweza kuwaelezea malengo ya Serikali katika kukuza Sekta zote mbili na kuona namna za kukuza Sekta hizo.

"hii yote imelenga katika kusikiliza changamoto zao mbalimbali pamoja na maoni yao, katika kuimarisha Sekta hii na ndio mana leo tumekutana na Uongozi wa Benki ya Equity ili kuangalia namna gani wafugaji na wavuvi wanaweza pata mikopo ili waweze kutanua wigo wa shughuli zao za biashara" amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru 

Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameweka wazi kuwa wafugaji wengi na wavuvi wengi wana mahitaji mbalimbali, ikiwemo vifaa vya kufanyia shughuli zao, kama vifaa vya kulimia Malisho, Vizimba pamoja na Miundombinu mbalimbali ambayo itawawezesha katika kutekeleza shughuli zao kwa urahisi zaidi.

Vilevile, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amewasihi Benki ya Equity kuendelea kutoa mikopo kwa wafugaji na wavuvi, ikiwemo wafugaji walioanza kufuga kisasa, kuwakopesha ili waweze kuendeleza shughuli zao Kisekta na hatimae waweze kukua katika shughuli zao za biashara.

Pia, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amebainisha kuwa Sekta hizo zina Mchango Mkubwa sana katika kuinua Pato la Taifa, na zinatakiwa kuchangia kwa asilimia 10% katika pato hilo ili kuingia kwenye Uchumi wa kati wa ngazi ya juu, na ameweka wazi kuwa Wizara inatambua michango ya Benki hizo katika kuwainua wafugaji na wavuvi kwa kuwapatia mikopo ambayo imekuwa msaada kwao, na amezishukuru Benki hizo na kuwaomba waendelee kuwawezesha Wafugaji na Wavuvi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Bi. Isabela Maganga amesema wao kama Benki ya Equity wameyapokea maoni ya Mheshimiwa Waziri na wataanza mchakato mapema wa kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanapata mikopo mbalimbali ili kuweza kuwainua katika shughuli zao.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO