WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI IMEFUNGUA MAFUNZO YA UFUATILIAJI WA VYOMBO VYA UVUVI (VESSEL MONITORING SYSTEM – VMS & AIS)
Na Herry Kilele – Bagamoyo, Pwani
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefungua mafunzo ya siku tano kwa wataalamu wa Sekta ya Uvuvi yenye lengo la kujenga uelewa wa matumizi ya mifumo ya ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi (VMS na AIS), hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kukabiliana na uvuvi haramu nchini.
Akizungumza Mei 5, 2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, akimuwakilisha Mkurugenzi wa Uvuvi, Bi. Lilian Ibengwe, Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisema:
“Tanzania imebahatika kuwa na rasilimali nyingi za uvuvi, jambo linaloiweka nchi miongoni mwa mataifa 10 yanayoongoza kwa uzalishaji wa samaki kutoka maji ya asili Barani Afrika.”
Alibainisha kuwa Sekta ya Uvuvi inachangia asilimia 1.8 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni 6.
Aidha, alieleza kuwa pamoja na mchango huo mkubwa, bado kuna changamoto ya kiwango cha chini cha ulaji wa samaki kwa Mtanzania, ambacho ni wastani wa kilo 7.9 kwa mtu kwa mwaka, ikilinganishwa na kiwango kinachopendekezwa kimataifa cha kilo 20.
Kwa mujibu wa Wizara, mifumo ya VMS na AIS ni nyenzo muhimu katika kufuatilia mienendo ya vyombo vya uvuvi, hususani katika kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu. Mifumo hiyo tayari imeunganishwa na vituo vya ufuatiliaji vilivyopo Dar es Salaam (Mvuvi House) na Zanzibar.
Bi Lilian ameelezwa kuwa Serikali ilianza kutumia mfumo wa VMS mwaka 2017 kwa meli za uvuvi wa kambamiti na imeendelea kupanua wigo wa matumizi yake kwa boti za ndani zenye urefu wa mita 10 na zaidi. Jitihada pia zinaendelea kuhakikisha wavuvi wadogo wanajumuishwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ECOFish na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji Tanzania (TASFAM).
Katika kuimarisha ufuatiliaji, Serikali imeunganisha mifumo ya VMS na AIS pamoja na teknolojia ya picha za satelaiti ili kubaini vyombo vinavyokiuka sheria. Vilevile, inaendelea na jitihada za kuunganisha mifumo hiyo kikanda na nchi jirani zikiwemo Kenya, Msumbiji na Shelisheli.
Bi. Lilian alieleza kuwa mifumo hiyo ni muhimu katika kulinda rasilimali za uvuvi kwa kuhakikisha ufuatiliaji wa vyombo unafanyika saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki.
Mafunzo hayo yamehusisha wataalamu wa mifumo ya ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi kutoka Kilwa, Mafia, Dar es Salaam, Tanga Mtwara, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority), TANTRADE. Pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi makao makuu Dodoma.
Washiriki wa mafunzo hayo wamehimizwa kutumia fursa hiyo kujifunza kwa kina na kuchangia mawazo yatakayosaidia kuboresha mifumo hiyo kwa manufaa ya Sekta ya Uvuvi na Taifa kwa ujumla.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wataalamu wa ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi kwa kizazi cha sasa na kijacho, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.




Maoni
Chapisha Maoni