VIJANA 3,004 WAOMBA MITAJI SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema jumla ya maombi 3,004 kwa ajili ya kuwawezesha mitaji vijana wanaojishughulisha na sekta za mifugo na uvuvi yamepokelewa na Wizara huku uchambuzi wa waombaji waliokidhi vigezo ukiendelea.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo leo Mei 26, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini Mhe. Ester Amos Bulaya (CCM) aliyehoji ni lini vijana wa Bunda watanufaika na Mradi wa Ufugaji Samaki wa Vizimba kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi?
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ilitangaza Machi 4, 2026 fursa ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 23.68 kwa ajili ya vijana wanaojihusisha na sekta za mifugo na uvuvi, hadi sasa jumla ya maombi 3,004 yamepokelewa kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo ya vijana kutoka Bunda, huku uchambuzi ukiendelea ili kupata waombaji waliokidhi vigezo” alisema Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilitekeleza awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo ya vizimba kwa vijana ambapo jumla ya vizimba 95 vilitolewa Mkoa wa Mara, na kati ya hivyo vizimba 20 vilielekezwa Wilaya ya Bunda.
Pamoja na hayo, ametoa rai kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda kuelekeza sehemu ya mikopo ya asilimia 10 ya vijana katika shughuli za ufugaji wa samaki kwa vizimba ili kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa buluu.


Maoni
Chapisha Maoni