TALIRI YAPONGEZWA KWA KUWEKEZA KWENYE UZALISHAJI WA MALISHO YA MIFUGO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa juhudi zake za kuwekeza katika uzalishaji wa malisho na mbegu bora za malisho ya mifugo, hatua aliyosema ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa malisho nchini.

Dkt. Madele ametoa pongezi hizo leo Mei 22, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kituo cha West Kilimanjaro kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Madele amesema sekta ya mifugo inaendelea kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa malisho kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, hivyo uwekezaji unaofanywa na TALIRI ni hatua muhimu ya kuimarisha ufugaji wenye tija na kuongeza uzalishaji.

Aidha, Dkt. Madele amewataka wataalamu wa TALIRI kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za ufugaji wa kisasa ili kuwawezesha wafugaji kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.

“Wafugaji wengi wamekuwa wakijiuliza ni wapi wanaweza kupata mbegu bora za malisho pamoja na mbari bora za mifugo. Uwepo wa huduma hizi kupitia TALIRI utatoa majawabu sahihi na kuongeza matumaini kwa wafugaji,” ameongeza Dkt. Madele.

Sambamba na hilo, Dkt. Madele amesema bado kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwaelimisha wafugaji kufuga mifugo inayolingana na uwezo wa rasilimali walizonazo ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kuepuka ufugaji usio na tija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Kaskazini, Dkt. Heriel Massawe amesema Kituo cha TALIRI West Kilimanjaro kimetenga ekari 300 ambazo zimewekewa uzio kwa ajili ya uzalishaji wa malisho na mbegu za malisho ya mifugo ili kusaidia wafugaji kupata huduma hiyo kwa urahisi na kuimarisha maendeleo ya sekta ya mifugo.

Dkt. Massawe amesema hatua hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa malisho bora, kuimarisha tafiti za mifugo na kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufugaji wenye tija.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Fabian Madele (wa tatu kushoto) akipokea maelezo kuhusu shamba darasa la uzalishaji wa malisho ya mifugo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Kaskazini Dkt. Heriel Massawe (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha TALIRI West Kilimanjaro kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Madele alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuzalisha malisho bora na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wenye tija ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa malisho inayochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mei 22, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO