SERIKALI YAENDELEA KUSISITIZA ULINZI NA USTAWI WA PUNDA AFRIKA
Na Chiku Makwai – Geita
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi punda kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya jamii, hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini wanaotegemea wanyama hao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani yaliyofanyika leo Mei 8, 2026 katika eneo la Mgusu mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, amesema siku hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua mchango mkubwa wa punda katika ustawi wa maisha na uchumi wa wananchi.
Aidha, Mhe. Komba amesema Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia haki za ustawi wa wanyama kama zilivyoainishwa katika Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008, ikiwemo haki ya kupata chakula na maji, kutoteswa, kupatiwa matibabu, kuishi bila hofu pamoja na kuwekwa katika mazingira yanayoruhusu kuonesha tabia zao za asili.
Amesisitiza kuwa wananchi na wafugaji wanapaswa kuhakikisha wanawatunza punda kwa kuzingatia misingi hiyo ili kuongeza tija pamoja na kulinda kizazi cha wanyama hao kwa manufaa ya sasa na ya baadaye. Pia amesema Serikali inaendelea kutekeleza Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2022 lililopitishwa na Umoja wa Afrika, linalopiga marufuku uchinjaji wa punda na biashara ya ngozi zake kwa kipindi cha miaka 15.
Vilevile, Mhe. Komba amezitaka taasisi za utafiti ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti zaidi kuhusu uzalishaji na uhifadhi wa punda nchini, huku akitoa wito kwa jamii na wadau wa ustawi wa wanyama kuendelea kushirikiana katika kulinda punda dhidi ya vitendo vinavyohatarisha uwepo wao barani Afrika.
Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo kutoka Shirika la INADES Formation Tanzania, Ndg. Charles Bukula amesema katika huduma za kliniki zilizotolewa wakati wa maadhimisho hayo, jumla ya punda 783 wamepatiwa matibabu mkoani Geita. Aidha, wanafunzi 5,105 pamoja na walimu 80 wamepatiwa elimu kuhusu ustawi wa punda kupitia programu za uhamasishaji zilizofanyika mashuleni.








Maoni
Chapisha Maoni